Main Title

source : Parstoday
Jumatano

20 Machi 2024

13:32:14
1445748

Qatar: Tuna matumaini ya kupatikana usitishaji vita Ukanda wa Ghaza

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar amesema kuwa, kumeshuhudiwa maendeleo mazuri kwenye mazungumzo ya kusimamisha vita na ana matumaini mazungumzo hayo yatazaa matunda mazuri.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRIB, Majid al Ansari amesema hayo jana jioni mjini Doha na kuongeza kuwa mazungumzo ya kusimamishwa vita na kubadilishana mateka kwa upatanishi wa Qatar na Misri yamejikita kwenye kufungua njia za kufikishwa misaada ya kibinadamu huko Ghaza.

Msemaji huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar amegusia pia shambulio la jana asubuhi lililofanywa na utawala wa Kizayuni ikiwa ni kukendeleza jinai za Israel za mauaji ya umati huko Rafah kusini mwa Ukanda wa Ghaza na kusisitiza kuwa, shambulio lolote kwenye eneo hilo ambalo lina wakimbizi wengi wa Palestina, litaathiri vibaya mazungumzo baina ya pande mbili.

Kwa mujibu wa televisheni ya al Mayadeen, jana asubuhi, utawala katili wa Israel ulifanya shambulizi la anga kwenye mji wa Rafah wa kusini mwa Ukanda wa Ghaza na kuua kwa umati Wapalestina wasiopungua 14 na kujeruhi makumi ya wengine kwa uungaji mkono kamili wa madola ya kibeberu hasa Marekani, Uingereza na Ujerumani.

342/