Main Title

source : Parstoday
Jumatano

20 Machi 2024

13:32:38
1445749

Rais wa Russia awapongeza Wairani kwa mnasaba wa Ramadhani na Mwaka Mpya

Rais wa Russia Vladimir Putin amelipongeza taifa la Iran kwa kwa minasaba miwili ya mwezi mtukfuu wa Ramadhani na kuwadiawaka mpya wa Kiirani wa Hijria Shamsiya ambao umeanza leo.

Ikulu ya Kremlin imesema katika taarifa yake kwamba Putin aliwapongeza wananchi wa Iran kwa mnasaba wa Mwezi wa Ramadhani na mwaka mpya wa Kiirani katika mazungumzo ya simu na Rais Ebrahim Raisi wa Iran siku ya Jumanne, huku akimtakia heri Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Seyyed Ali Khamenei.

Marais hao wawili walijadili ushirikiano baina ya nchi hizo mbili, ikiwa ni pamoja na upanuzi wa mahusiano ya kiuchumi na miradi mikubwa ya uwekezaji.

Putin ameashiria kukamilishwa kwa rasimu ya makubaliano ya ushirikiano wa kina kati ya Iran na Russia.

Akibainisha nukta hiyo amesema: "Kufanyika kwa mafanikio kwa mkutano wa kamisheni ya pamoja ya ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizi mbili mjini Tehran, pamoja na ukuaji wa asilimia 77 wa biashara ya bidhaa kati ya Iran na Russia ni dalili chanya za kuimarika kwa ushirikiano wa Tehran na Moscow."

Putin pia amesema uwepo wa Iran na Russia katika Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai na BRICS ni fursa adhimu ya kuzidisha maingiliano kati ya pande mbili.

Marais hao wawili walijadili zaidi hali mbaya katika Ukanda wa Gaza huku kukiwa na vita vya mauaji ya kimbari vinavyoendelezwa na Israel, wakielezea wasiwasi wao juu ya ongezeko la idadi ya wahanga.

Rais Putin amesema Iran na Russia zimechukua misimamo sawa kuhusu suala la mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza, akiongeza kuwa Moscow iko tayari kushirikiana zaidi na Tehran linapokuja suala la Palestina.

Kwa upande wake Rais wa Iran kwa mara nyingine ametoa pongezi kwa Putin kwa kuchaguliwa tena, akielezea matumaini yake kuwa serikali mpya ya Russia itaweka msingi mwafaka wa upanuzi wa uhusiano na ushirikiano wenye manufaa kati ya mataifa hayo mawili katika nyanja mbalimbali.

Alipongeza makubaliano yaliyofanywa kati ya pande hizo mbili, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa reli ya Rasht-Astara, kama "msingi unaofaa" wa kuimarisha ushirikiano wa nchi mbili, hasa kwa ajili ya kukuza uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya nchi hizo mbili.

Raisi amesisitiza ulazima wa kuchukuliwa hatua madhubuti za kimataifa ili kukomesha mashambulizi ya jinai ya utawala wa Israel huko Gaza, pamoja na kuondoa vizingiti na kutoa misaada ya kibinadamu kwa watu wa eneo hilo linalozingirwa.