Main Title

source : Parstoday
Jumatano

20 Machi 2024

13:34:08
1445751

Polisi ya Brazil yamshtaki rais wa zamani Bolsonaro kwa kughushi cheti cha chanjo ya COVID

Polisi ya Brazil imependekeza rais wa zamani wa nchi hiyo Jair Bolsonaro ashtakiwe kwa kughushi cheti chake cha chanjo ya COVID.

Shtaka la Polisi ya Shirikisho lilitolewa na Mahakama ya Juu ya Brazil siku ya Jumanne, kufuatia uchunguzi ulioanza mwaka jana. Uchunguzi huo ni mojawapo ya kesi kadhaa zilizofunguliwa dhidi ya mwanasiasa huyo wa mrengo wa kulia tangu muhula wake wa uongozi ulipomalizika Desemba 2022.Bolsonaro, mwenye umri wa miaka 61, ambaye hapo awali alisema hakuchanjwa, amekuwa akichunguzwa tangu mwaka jana kwa tuhuma kwamba aliamuru wasaidizi wake kupotosha rekodi yake ya afya ili kumruhusu kusafiri kimataifa. Wakati wa urais wake alishutumiwa vikali kwa kupuuzilia mbali hatari ya janga la Corona.

Polisi ya Shirikisho nchini Brazil imeeleza katika ripoti ya kurasa 231 kwamba Bolsonaro na watu wengine 16 walikuwa wamepanga njama ya kutoa "vyeti bandia ili kupata faida zisizofaa" wakati virusi vikiendelea.Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kuna uwezekano wa kiongozi huyo kushtakiwa kwa kushiriki katika uhalifu na "kuingiza taarifa za uongo kwenye mfumo wa umma", makosa ambayo, yote mawili yana adhabu ya kifungo jela. Sasa ni juu ya afisi ya Mwanasheria Mkuu kuamua kama itamfungulia mashtaka mkuu huyo wa zamani wa nchi au la. Timu ya utetezi ya Bolsonaro imesema, rais huyo wa zamani wa Brazil aliyekuwa maarufu kama 'Trump wa Brazil' kutokana na hatua za ajabuajabu alizokuwa akichukua alipokuweko madarakani, hakujua kama kuna mshauri wake yeyote aliyekuwa ametengeneza cheti bandia cha chanjo kwa ajili yake na kwamba yeyote aliyefanya hivyo alitenda hayo kwa hiari yake mwenyewe. Mnamo mwezi Januari, Ofisi ya Mdhibiti Mkuu wa Brazil ilithibitisha kuwa cheti cha chanjo ya COVID cha Bolsonaro kilighushiwa, lakini ilipendekeza kufungwa kwa kesi hiyo kwa sababu ya kukosekana ushahidi wa kutosha juu ya nani aliyeingiza taarifa hizo za uongo.../

342/