Main Title

source : Parstoday
Jumatano

20 Machi 2024

13:36:38
1445756

Iran yaonya kuhusu hatua za Wazayuni dhidi ya Wapalestina wanaokwenda kusali Msikiti wa Al-Aqsa

Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametahadharisha kuhusu vitendo vyovyote vya kichokozi vinavyoweza kufanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika eneo la Quds Tukufu na Msikiti wa Al-Aqsa dhidi ya Waislamu Wapalestina wanaokwenda kusali katika msikiti huo wakati huu wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Tasnim, Seyed Ebrahim Raisi, ameyasema hayo katika ujumbe aliowatumia viongozi wa nchi za Kiislamu na kusisitiza kuwa, kuendelea mauaji ya kimbari huko Ghaza na jinai za kivita za utawala wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi wa Palestina bila shaka ndio masuala makuu yanayoshughulisha Umma wa Kiislamu. Amefafanua kuwa, moja ya malengo hatari ya utawala bandia wa Israel ni kufuuta athari zote za maisha na utambulisho wa Wapalestina, kuweka mazingira ya msambaratiko wa kijamii na kiraia na kuwahamisha kwa nguvu wakazi wa Ukanda wa Ghaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan kuelekea nchi jirani. Raisi ameongeza kuwa: utawala wa Kizayuni unatekeleza kwa makusudi sera ya kuliangamiza moja kwa moja taifa la Palestina na utambulisho wake kwa kushirikiana na Marekani.Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, jukumu la kuzuia maafa ya kibinadamu huko Palestina na Ghaza liko mikononi mwa taasisi za kimataifa hususan Umoja wa Mataifa, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC na Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu na akabainisha kuwa: katika mazingira haya nyeti na hasasi, na katika mwezi mtukufu wa Ramadhani, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatoa indhari juu ya kuendelea ukatili wa mauaji ya wazi kabisa ya kimbari yanayofanywa dhidi ya taifa, na kwa mara nyingine tena inatilia mkazo ulazima wa kuchukuliwa hatua madhubuti na athirifu za kukomesha mauaji hayo, kuondolewa mzingiro kikamilifu na kukabidhiwa kwenye vyombo vya sheria wazayuni watoaji amri na watekelezaji wa jinai zinazofanywa na utawala bandia wa Israel.

 Hivi karibuni jeshi la Israel lilifunga barabara zinazoelekea Msikiti wa Al-Aqsa ili kuwazuia waumini Wapalestina kuingia msikitini humo. Hayo yanajiri huku Wizara ya Afya ya Palestina katika Ukanda wa Ghaza ikiripoti kuwa, katika saa 24 zilizopita, Wapalestina 104 wameuawa shahidi na wengine 162 wamejeruhiwa katika mashambulio yanayoendelea kufanywa mtawalia na jeshi la utawala wa Kizayuni katika eneo hilo.

Kwa mujibu wa taarifa ya wizara hiyo, idadi ya Wapalestina waliouawa shahidi kutokana na mashambulio ya kinyama ya jeshi la Israel tangu Oktoba 7 hadi sasa, imeshapindukia 31,923 na waliojeruhiwa pia ni zaidi ya 74,096.../


342/