Main Title

source : Parstoday
Jumatano

20 Machi 2024

13:37:26
1445757

Maadhimisho ya kupitishwa kwa sheria ya kutaifishwa kwa sekta ya mafuta ya Iran

Siku ya mwisho katika kalenda ya Hijria Shamsia ya Iran ambayo ilikuwa jana ni maarufu kama "Siku ya Kutaifisha Sekta ya Mafuta". Katika siku hii, miaka 73 iliyopita baada ya vuta nikuvute na mapambano ya wananchi wa Iran dhidi ya mkoloni Mwingereza na utawala kibaraka wa mfalme hapa nchini, hatimaye wabunge wa Bunge la Taifa walipitisha muswada wa kutaifisha sekta ya mafuta nchini.

Kuidhinishwa kwa sheria ya kutaifisha sekta ya mafuta ya Iran tarehe 29 Isfand 1329 Hijria Shamsia (Aprili 1951) kulikuwa  ni hatua ya mabadiliko katika historia ya kisiasa na kiuchumi ya wananchi wa Iran ili kuuokoa utajiri wa taifa kutoka mikononi mwa ajinabi waporaji.

Katika zama hizo, Iran ilikuwa mzalishaji mkubwa wa mafuta Asia Magharibi na baada ya Marekani, Venezuela na Umoja wa Kisovieti ilikuwa nchi ya nne kwa uzalishaji wa mafuta ghafi duniani. Katika kipindi hichom Uingereza ilipata fursa ya kunyonya na kupora mafuta ya kusini mwa Iran, na Urusi na Marekani ziliutazama utajiri wa mafuta wa Iran jicho la tamaa. Hivyo wakoloni walikuwa wakivutana kupora utajiri wa mafuta ya Iran.Wakati serikali ya Waziri Mkuu wa wakati huo wa Iran Mohammad Mossadegh ilipoweka utekelezwaji wa sheria ya kutaifisha sekta ya mafuta kwenye kilele cha ajenda ya serikali mwezi Aprili 1951, hujuma na njama dhidi ya Iran zilizidi kudhihirika. Mapinduzi ya Marekani na Uingereza mnamo Agosti 1953 dhidi ya serikali ya Mossadegh yalikuwa sehemu ya njama hizi.

Baada ya kupinduliwa serikali ya Mossadegh; makampuni ya mafuta yakiwemo British Petroleum, Shell na California na Texas ya Marekani na Uingereza yaliingia katika uwanja wa unyonyaji na uporaji wa mafuta ya Iran ili udhibiti wao wa sekta ya mafuta ya Iran ubaki licha ya kutaifishwa kwa sekta hii.

Lakini baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran mwaka 1979, mikataba yote ya kigeni, ukiwemo mkataba wa 1954 ambao ni maarufu kama Consortium Agreement ilifutwa.

Kimsingi ni kuwa baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, haki ya  utafutaji, uchimbaji, usafishaji na usafirishaji wa mafuta ilikuwa sasa mikononi mwa Kampuni ya Kitaifa ya Mafuta ya Iran.

Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na kutekwa kiota cha kijasusi cha Marekani yaani ubalozi wa Marekani mjini Tehran, miezi miwili baadaye, vikwazo vya kwanza vya Marekani viliwekwa dhidi ya sekta ya mafuta ya Iran. Marekani ilijua vyema kwamba ili kuudhuru uchumi wa Iran, ilibidi ilenge sekta ya mafuta kwa vikwazo.Kwa hakika, hadi miaka ishirini baada ya mapinduzi, vikwazo dhidi ya Iran vilikuwa hasa vikwazo vya mafuta.

Lengo la maadui katika kuweka vikwazo dhidi ya sekta ya mafuta ya Iran lilikuwa ni kukata uuzaji nje wa mafuta ili kuusambaratisha uchumi wa Iran, na lingine lilikuwa ni kudhoofisha sekta hii na kupunguza uwezo wa uzalishaji wa nchi kwa kuzuia kuingizwa vifaa na huduma zinazohitajika.

Kwa hivyo, uzalishaji wa mafuta wa Iran, ambao unategemea sana  vifaa maalum, ulikuwa hatarini. Hivyo kwa mara nyingine tena kwa usaidizi wenye bidii, uwezo na werevu wa wataalamu wa Iran,  vifaa vya vinavyohitajika katika sekta ya mafuta vilianza kuundwa hapa nchini na hivi sasa karibu 85% ya  vifaa hivi vimezalishwa nchini Iran na vilivyosalia navyo kwa hima ya wataalamu vitaanza kuzalishwa hapa nchini.

Moja ya mafanikio muhimu ya sekta ya mafuta na gesi baada ya mapinduzi ya Kiislamu ni maendeleo ya maeneo ya mafuta na gesi, hasa eneo la Pars Kusini, ambalo ni eneo kubwa zaidi lenye hifadhi ya gesi asilia duniani.Bila shaka sekta ya nishati hususan mafuta na gesi ndiyo sekta muhimu zaidi ya uchumi wa Iran, kwa sababu sehemu kubwa ya mapato ya nchi yanatolewa na sekta hii. Baada ya Venezuela, Saudi Arabia na Kanada, Iran ina hifadhi ya nne kubwa zaidi ya mafuta duniani ikiwa na mapipa bilioni 160. Iran pia ina akiba ya pili ya gesi iliyothibitishwa ulimwenguni, na akiba ya gesi ya Iran ilikuwa katika kiwango cha mita za ujazo trilioni 33.98 mnamo 2022. Matokeo ya ugunduzi wa mafuta na gesi yanaonesha kuwa asilimia 25 ya akiba ya mafuta iligunduliwa katika kipindi cha baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, huku katika sekta ya gesi, uvumbuzi mwingi (75%) ulihusiana na kipindi cha baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Kwa mujibu wa maono ya tasnia ya mafuta na gesi ya Iran katika kipindi cha miaka miwili ijayo, Iran kwa kujitegemea kwa kiwango kikubwa, itakuwa kitovu cha mabadilishano ya nishati (mafuta na gesi) ya dunia na katika maingiliano ya kimataifa yenye ufanisi na nchi nyingine, hasa wahusika wakuu katika uwanja wa nishati, ikijumuisha maeneo ya uzalishaji, usambazaji, huduma na matumizi ya nishati.

342/