Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

21 Machi 2024

13:29:23
1445932

Iran yalaani kimya cha dunia mkabala wa jinai za Israel huko Gaza

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa mwito wa kusitishwa uungaji mkono kwa jinai na mauaji yanayofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina.

Katika ujumbe alioutuma kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X (Twitter), Nasser Kan'ani amesema: Unyama na ukatili wa utawala wa Kizayuni unaendelea katika Ukanda wa Gaza mbele ya macho ya ulimwengu; siku 167 za vita zimepita na taasisi za kimataifa zimeshindwa kuchukua hatua zozote za maana. Dunia imebaki kuzungumza tu, lakini haijachukua hatua yoyote.

Amesema inasikitisha kuwaona walimwengu wamenyamazia kimya jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu zinazofanywa na Wazayuni dhidi ya Wapalestina wasio na ulinzi wa Ukanda wa Gaza.

"Maneno hayawezi kueleza ukubwa wa ukatili wa kuchupa mipaka unaofanyika (Gaza) machoni la jamii ya kimataifa," ameongeza Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran.

Kan'ani ameashiria mzingiro dhidi ya Hospitali ya al-Shifa kwa siku ya nne mfufulizo na kueleza kuwa, waungaji mkono, na wale wanaonyamazia kimya jinai za kinyama na za kutisha za Wazayuni huko Gaza wanapasa kufedheheka.

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran kwa mara nyingine tena amesisitiza kuwa, jamii ya kimataifa ina wajibu kuhusu hali chungu ya Ukanda wa Gaza, na kuutaka Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama kutekeleza wajibu wao kimataifa ili kuzuia kuendelea jinai za kivita zinazofanywa na utawala ghasibu wa Israel. Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Palestina, watu karibu elfu 32 wameuliwa shahidi hadi sasa tangu utawala wa Kizayuni uanzishe vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Ukanda wa Gaza Oktoba 7 mwaka jana. Katika hatua nyingine, Benki ya Dunia imetahadharisha kuwa, asilimia 50 ya wakazi wa Gaza wapo katika hatari ya kupoteza maisha kutokana na makali ya njaa, huku kiwango cha uhaba wa chakula kikifikia kiwango cha kutisha. Taasisi hiyo ya kifedha yenye makao yake mjini Washington ilisema hayo jana katika ripoti yake na kueleza kuwa: Huku nusu ya wakazi wote wa Gaza wakiwajihiwa na hatari ya kufa njaa, wakiwemo watoto na wakongwe, Kundi ya Benki ya Dunia linatoa mwito wa kuchukuliwa hatua za dharura ili kuokoa maisha.

342/