Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

22 Machi 2024

14:22:31
1446121

Uchambuzi wa vita vya Gaza katika hotuba ya Nowruz ya kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu

Katika hotuba yake ya siku ya kwanza ya mwaka mpya wa 1403 Hijria Shamsia, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei, amesema suala la Palestina na Gaza ni suala la daraja ya kwanza la kimataifa na kusisitiza kuwa: Kadhia ya Gaza imeonesha jinsi ulimwengu eti uliostaarabika na unaodai kutetea haki za binadamu, unavyofanya dhulma kubwa dhidi ya watu wa Gaza.

Katika hotuba hiyo, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia suala la Palestina katika pande kadhaa. Upande wa kwanza ni ukosoaji wa madai ya kutetea haki za binadamu ya nchi za Magharibi. Takriban watu 32,000 wameuawa shahidi na utawala wa Kizayuni wa Israel huko Gaza, maisha ya watu yameharibiwa katika eneo hilo, na hata baadhi ya viongozi wa nchi za Magharibi wanaendelea kueleza wasiwasi wao na kuonya kuhusu hali mbaya ya binadamu katika ukanda huo. Katika mkondo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, amekuwa akisisitiza mara kwa mara kuwa, kinachofanywa na Israel huko Gaza ni kielelezo cha mauaji ya kimbari. Hata hivyo, inaonekana kuwa haki za binadamu zinazodaiwa na nchi za Magharibi haziwajumuishi watu wa Gaza, na nchi hizo zimechangia katika kuzidisha mgogoro wa binadamu katika eneo hilo la Palestina.

kuhusuiana na ukweli huu Ayatullah Khamenei amesema: "Kadhia ya Gaza na mauaji ya zaidi ya watu elfu 30,000, wanawake, watoto, wazee, vijana na hata wagonjwa, mbele ya macho ya ulimwengu eti uliostaarabika na unaodai kutetea haki za binadamu, ni kielelezo cha dhulma na giza linalotawala nchi za Magharibi." 

Katika upande wa pili, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia haki na msimamo sahihi wa makundi ya mapambano na Muqawama katika eneo la Asia Magharibi. Msimamo huo sahihi unatokana na kwamba kambi ya Muqawama haikunyamaza kimya mbele ya jinai na uhalifu inaofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel, ilhali ulimwengu wa Magharibin si tu kwamba umenyamaza kimya, bali pia ni mshirika katika uhalifu na jinai hizo.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake ya mwaka mpya, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia mgogoro na udhaifu unaoutafuna kwa ndani utawala ghasibu wa Israel. Kwa upande mmoja, vita vya Gaza vimeonesha migogoro ya ndani ya utawala wa Kizayuni, kama vile hitilafu na mpasuko mkubwa wa kisiasa, misimamo mikali na hali ya kutoridhika iliyoenea baina ya Wazayuni. Katika upande mwingine, vita hivi vimethibitisha kwamba, Gaza ni kinamasi kwa utawala wa Kizayuni, ambacho hauwezi kujiondoa ndani yake. Ayatullah Khamenei amesema: "Kuingia utawala wa Kizayuni katika vita vya Gaza, kumeutumbukiza utawala huo kwenye kinamasi na kuufanya ushindwe, bila ya kijali kama utaondoka au kubakia katika eneo hilo." 

Sehemu nyingine ya hotuba ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu imeeleza uhakika kwamba vita vya Gaza vimezidisha chuki ya walimwengu dhidi ya Marekani. Kuhusiana na suala hili Ayatullah Ali Khamenei amesema: "Marekani imechagua nafasi mbaya zaidi katika kadhia ya Gaza. Imejiweka katika nafasi ya kuchukiwa na walimwengu wote. Watu wanaofanya maandamano ya kuitetea Palestina katika mitaa ya London, Paris na nchi nyingine za Ulaya na Marekani kwenyewe, kwa hakika wanatangaza chuki dhidi ya Marekani."

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, mahesabu potofu ya Marekani katika kadhia ya Gaza yameifanya nchi hiyo ichukiwe kote duniani na kuongezeka chuki dhidi yake mara kumi katika eneo la Asia Magharibi.