Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

23 Machi 2024

14:31:08
1446298

Iran yalaani shambulizi la kigaidi lililoua makumi ya watu nchini Russia

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani vikali shambulio la kigaidi lililoua na kujeruhi makumi ya watu katika mji mkuu wa Russia, Moscow.

Nasser Kan'ani, Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, shambulio hilo la kinyama nchini Russia kwa mara nyingine tena limeonyesha kuwa, ugaidi na uchupaji mipaka ni tishio kwa ulimwengu mzima.

Sanjari na kutoa mkono wa pole na kutangaza kuwa pamoja na serikali na wananchi wa Russia kufuatia hujuma hiyo, Kan'ani ameeleza kuwa, shambulio hilo limethibitisha kwamba, kuna haja ya kuweko vita na mapambano athirifu sambamba na ushirikiano wa jamii ya kimataifa dhidi ugaidi.

Aidha Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran sanjari na kulaani vikali shambulio hilo, amesisitiza kuwa vita dhidi ya ugaidi vinahitaji hatua na ushirikiano madhubuti wa jamii ya kimataifa.  

Kwa akali watu 60 wameuawa katika shambulio hilo la kigaidi la usiku wa kuamkia leo katika ukumbi mmoja wa tamasha viungani mwa Moscow, mji mkuu wa Russia. Bila kutoa ushahidi wowote, kundi la kigaidi la ISIS (Daesh) limetengaza kuhusika na hujuma hiyo.Video moja iliyosambaa mitandaoni inaonyesha watu wanne waliojizatiti kwa bunduki ya otomatiki wakiwamiminia risasi watu waliokuwa wamekusanyika kwenye ukumbi huo, dakika dakika chache baada ya kujiri mripuko na moto mkubwa kusambaa ukumbini hapo. Kwa mujibu wa Kamati ya Uchunguzi ya Russia, mbali na watu 60 kuuawa, wengine wasiopungua 150 wamejeruhiwa kwenye hujuma hiyo ya kigaidi iliyolenga ukumbi wa 'Crocus City Music Hall' jijini Moscow. Meya wa Moscow, Sergei Sobyanin amelitaja shambulio hilo kama 'janga baya la kuogofya'. Kadhalika Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amelaani shambulio hilo, huku Baraza la Usalama la umoja huo likisistiza kuwa kuna haja ya kuwajibishwa wahusika wa jinai hiyo.

342/