Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

23 Machi 2024

14:31:42
1446299

Washukiwa wanne wakuu wa shambulizi la kigaidi la Moscow wakamatwa, idadi ya wahanga imefika 93

Ikulu ya Rais wa Russia, Kremlin, imetangaza habari ya kukamatwa watu 11, wakiwemo wanne waliohusika moja kwa moja katika shambulio lililolenga jumba la tamasha mjini Moscow jana Ijumaa, na kuua makumi ya watu.

Kremlin imesema kuwa Huduma ya Usalama ya Shirikisho inafanya kazi kubaini upande ulioshirikiana na magaidi waliofanya shambulio hilo.

Kamati ya Uchunguzi ya Russia imetangaza mapema leo Jumamosi, ikinukuu data za awali, kwamba kwa uchache watu 93 waliuawa katika shambulio hilo, na kuonya kwamba idadi ya waliouawa huenda ikaongezeka.

Kamati hiyo imesema, washukiwa hao wamekamatwa katika eneo la Bryansk la Russia, karibu na mpaka wa Ukraine.

Idara ya Usalama ya Urusi imesema washukiwa wa shambulio hilo walipanga kuvuka mpaka na walikuwa wakiwasiliana na watu wengine upande wa Ukraine.

Shirika la habari la TASS limemnukuu Katibu wa Baraza la Usalama la Russia , Nikolai Patrushev, mshirika mashuhuri wa Rais Vladimir Putin, akisema leo kwamba waliohusika na shambulio la tamasha karibu na Moscow wataadhibiwa.

Patrushev ameongeza kuwa: "Shambulio hilo limeonyesha kiwango cha tishio la ugaidi kwa Russia."Awali, kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) ilidai kuhusika na shambulio hilo, na kusema katika taarifa iliyotumwa kwenye mtandao wa Telegram kwamba wapiganaji wake walishambulia mkusanyiko mkubwa nje kidogo ya mji mkuu wa Russia, Moscow, na kwamba wamerejea kwenye ngome zao salama. Katika ngazi ya kimataifa, Umoja wa Mataifa umeeleza kusikitishwa kwake na shambulio hilo. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Nasser Kan'ani amesema kuwa, shambulio hilo la kinyama nchini Russia kwa mara nyingine tena limeonyesha kuwa, ugaidi na uchupaji mipaka ni tishio kwa ulimwengu mzima. Video iliyosambaa mitandaoni inaonyesha watu wanne waliojizatiti kwa bunduki ya otomatiki wakiwamiminia risasi watu waliokuwa wamekusanyika kwenye ukumbi wa tamasha kwenye viunga vya mji wa Moscow, dakika dakika chache baada ya kujiri mripuko na moto mkubwa kusambaa ukumbini hapo.

342/