Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

23 Machi 2024

14:32:47
1446301

Russia: Umoja wa Ulaya unahusika na mashambulizi ya kigaidi ya Ukraine dhidi ya Warusi

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia, Maria Zakharova, amesema kuwa mipango ya Umoja wa Ulaya ya kutenga euro bilioni 50 kama msaada wa kifedha na kiuchumi kwa ajili ya Ukraine "haitauokoa utawala wa Kinazi huko Kiev."

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amesema kuwa uongozi wa Umoja wa Ulaya, unaoipatia Ukraine silaha na kuichochea kutekeleza uhalifu, lazima ubeba dhima sawa na uongozi wa Ukraine kwa vitendo vya kigaidi vinavyofanywa dhidi ya raia wa Russia.

Zakharova amesema katika maoni yaliyochapishwa kwenye tovuti rasmi ya wizara hiyo kwamba "kwa msukumo wa Magharibi, Waukraine hawasiti kufanya vitendo vya kigaidi dhidi ya miundombinu ya kiraia na wakazi wenye amani katika miji ya Russia."Ameongeza kuwa: "Uongozi wa sasa wa Umoja wa Ulaya na nchi wanachama wake, ambazo hutoa misaada ya silaha kwa Kiev na kuichochea kufanya uhalifu wa kimataifa, unapaswa kubeba majukumu na kuwajibishwa pamoja na Ukraine kwa vitendo hivi." Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje Russia amesisitiza kuwa mipango ya Umoja wa Ulaya ya kutenga euro bilioni 50 za msaada wa kifedha na kiuchumi kwa Ukraine "haitauokoa utawala wa Kinazi wa Kiev." Ukraine imepokea msaada mkubwa wa kifedha na kijeshi kutoka nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani, Uingereza, na nchi kubwa za Ulaya, tangu kuanza vita baina ya nchi hiyo na Russia.

342/