Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

23 Machi 2024

14:34:50
1446304

Russia, China zalipigia turufu azimio la US kuhusu Gaza lenye kuunga mkono Israel

Azimio la Marekani la kutaka kusitishwa kwa mapigano huko Gaza linalohusishwa na mpango wa wafungwa na mateka limepingwa na Russia na China katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kutokana na msimamo wake wa kuiunga mkono Israel.

Wajumbe kumi na moja wa Baraza la Usalama walipiga kura kwa azimio hilo Ijumaa ambapo Russia, China na Algeria zilipiga kura dhidi yake na Guyana haikupiga kura. Kama wanachama wa kudumu wa baraza la usalama kura za Russia na China zilihesabiwa kama kura ya turufu.

Kabla ya upigaji kura, mjumbe wa Russia katika Umoja wa Mataifa, Vasily Nebenzya, alidokeza kwamba Marekani ilikuwa imepiga kura ya turufu maazimio manne ya awali ya kutaka kusitishwa kwa vita tangu kuanza kwa vita vya mauaji ya kimbari vya Israel dhidi ya Gaza mnamo tarehe 7 Oktoba, na akabainisha kuwa azimio la Marekani halikudai moja kwa moja kusitishwa kwa vita.

Balozi wa China katika Umoja wa Mataifa Zhang Jun amesema Baraza la Usalama "limeburuza miguu" kwa muda mrefu sana kuhusu suala la kusitishwa kwa mapigano mara moja huko Gaza.

Aliongeza kuwa azimio hilo lililopendekezwa na Marekani lilkwepa suala la usitishaji vita, halikuwa wazi na liliepuka kutoa wito wa kusitishwa kwa mapigano mara moja.

Riyad Mansour, balozi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa, amesema rasimu ya azimio la Marekani ilikataliwa kwa "sababu za wazi", akiitaja kuwa ya "upande mmoja" na kubainisha kuwa iliitaja Israel mara moja tu.

Aliwaambia waandishi wa habari, "Tunakataa kudai kile kinachotokea kama suala la ugaidi. Ni mauaji ya kimbari dhidi ya wakazi wote wa Wapalestina katika Ukanda wa Gaza."

 342/