Main Title

source : Parstoday
Jumapili

24 Machi 2024

14:19:51
1446522

Katibu Mkuu wa UN alaani Israel kuzuia malori ya misaada yasiingie Ghaza, 7,000 yamepanga safu Misri

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani kuzuiwa kwa malori ya misaada yaliyoko katika upande wa Misri wa mpaka na Ukanda wa Ghaza, akiielezea hatua hiyo kuwa inasababisha "ghadhabu ya kimaadili."

Akiwa katika ziara yake katika kivuko cha mpaka cha Rafah jana Jumamosi, Guterres amesisitiza udharura wa utawala wa Kizayuni wa Israel kudhamini upatikanaji wa misaada ya kibinadamu bila kikomo katika eneo lote la Ghaza na kutoa wito wa kusitishwa mara moja mapigano kwa sababu za kibinadamu. Katibu Mkuu wa UN amesema: "hapa kutoka kwenye kivuko hiki, tunaona huzuni na uchungu wa yote hayo. Msururu mrefu wa malori ya misaada yaliyozuiwa upande mmoja wa malango na kivuli kirefu cha njaa kwa upande mwingine. Hiyo ni zaidi ya janga. Ni hasira ya kimaadili." Akiwa katika safari hiyo ya kutembelea kivuko cha Rafah, Guterres ameonya juu ya matokeo mabaya ya kuendelea kuzuiwa misaada, akisema, "ni wakati wa kuimimina misaada ya kuokoa maisha Ghaza. Chaguo liko wazi: ama kuongezeka au ni njaa." Ziara hiyo ya Katibu Mkuu wa UN inafanyika sambamba na kuongezeka mashinikizo ya kimataifa kwa utawala wa Kizayuni wa Israel ya kuutaka uruhusu misaada ya kibinadamu kuingia Ghaza, ambayo iko katika hatari ya kukumbwa na baa la njaa huku kukiwa na uhaba mkubwa wa chakula na maji.Kabla ya kusimama mpakani, ambako alikutana na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wa kutoa misaada ya kibinadamu, Guterres alitua Al Arish kaskazini mwa Sinai nchini Misri, ambako misaada mingi ya kimataifa kwa Ghaza inatolewa na kuhifadhiwa. Gavana wa eneo hilo Mohamed Shusha alimwambia Guterres kwamba malori yapatayo 7,000 yalikuwa yakingoja Sinai Kaskazini kupeleka misaada Ghaza, lakini yamezuiliwa kwa sababu ya taratibu za ukaguzi zinazotakiwa na utawala wa Kizayuni wa Israel. Wakati huohuo, Philippe Lazzarini, Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina UNRWA amesema, utawala wa Kizayuni wa Israel umezuia msafara wa chakula kwa mara ya pili wiki hii. Katika ujumbe alioandika kwenye mtandao wa X, Lazzarini amebainisha kuwa mara ya mwisho UNRWA iliweza kupeleka misaada kaskazini mwa Ghaza, ambako njaa inaenea, ilikuwa miezi miwili iliyopita. Mkuu wa UNRWA amesisitiza kwa kusema: "nimeeleza mara nyingi: hii ni njaa ya kusababishwa na mwanadamu na ni baa la njaa linalozidi kukaribia lakini linaweza kuepukwa".

342/