Main Title

source : Parstoday
Jumapili

24 Machi 2024

14:21:08
1446525

Ndege ya kivita isiyo na rubani ya Iran ijulikanayo kama 'Gaza' yavuma kimataifa

Iran imeanza kusambaza bidhaa zake za kijeshi na ulinzi kimataifa, huku gazeti moja la Marekani likisema kuwa sekta ya ulinzi ya Iran imeingia rasmi katika soko la kimataifa kwa kushiriki katika Maonyesho ya Kimataifa ya Silaha ya Doha nchini Qatar ambapo imeonyesha ndege ya kisasa ya kivita isiyo na rubani iliyopewa jina la 'Gaza'.

Gazeti la Wall Street Journal liliripoti Jumamosi kuwa ndege hiyo isiyo na rubani ya Gaza ilionyeshwa hivi karibuni kwenye maonyesho  hayo Doha. Hii ni mara ya kwanza kwa ndege hiyo isiyo na rubani kuonyeshwa nje ya Iran.

Ripoti hiyo imesema, ndege hiyo ya kivita isiyo na rubani au droni ina uwezo wa kuruka umbali wa maili 1,243, ina mabawa ya futi 68 na kiunganishi cha satelaiti huku ikiwa na uwezo wa kubeba mabomu 13 yanayoongozwa kwa usahihi mkubwa. Aidha gazeti hilo limeandika droni hiyo ya Iran  ni "tishio kwa maslahi ya Marekani na waitifaki wake."

Gazeti la Wall Street Journali pia limeandika kuwa  droni hiyo ya kisasa ya Iran ni hasimu mkuu wa droni ya kisasa ya kivita iliyoundwa Marekani ya MQ-9A Reaper.Katika maonyesho hayo ya  Doha, Iran imewasilisha zana mbali mbali za kijeshi na ulinzi ikiwa ni pamoja na makombora ya ulinzi wa anga, maroketi ya kurusha satalaiti katika anga za mbali, makombora mapya ya kuzamisha meli za kivita na mifumo ya rada.

Tangu kumalizika muda wa vikwazo vya silaha vya miaka 13 vya Umoja wa Mataifa mwezi Oktoba, Iran imeongeza uuzaji wa bidhaa zake za ulinzi kwenye soko la kimataifa.

Naibu Waziri wa Ulinzi wa Iran Mahdi Farahi alisema mwezi Novemba kwamba Iran iliuza zana za kivita zenye thamani ya takriban dola bilioni 1 kuanzia Machi 2022 hadi Machi 2023, mara tatu zaidi ya mwaka uliotangulia.


342/