Main Title

source : Parstoday
Jumapili

24 Machi 2024

14:21:31
1446526

Iran: Tuko pamoja na Russia baada ya shambulio la kigaidi la Moscow

Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa mwito kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua kali za kuwaadhibu magaidi waliohusika na shambulio la kigaidi kwenye jumba moja la starehe katika viunga vya Moscow, mji mkuu wa Russia.

Katika ujumbe wake kwa Rais Vladimir Putin wa jana Jumamosi, Rais Raisi ametoa mkono wa pole kwa serikali na wananchi wa Russia kwa kuuawa watu wasio na hatia na amelaani vikali shambulizi hilo la kigaidi.

Vilevile Rais Raisi pia ametilia mkazo uungaji mkono wa Iran kwa juhudi za serikali ya Russia za kudumisha usalama ndani ya nchi hiyo.

Magaidi wenye silaha waliokuwa wamejificha, walifyatua risasi katika Ukumbi wa Starehe wa Jiji la Crocus uliokuwa umejaa watu kwenye kitongoji cha Krasnogorsk cha kaskazini mwa Moscow Ijumaa jioni. Shambulizi hilo linahesabiwa kuwa hujuma mbaya zaidi ya kigaidi kuwahi kutokea Russia kwa uchache katika kipindi cha miaka kumi iliyopita.

Hii ni katika hali ambayo, Ikulu ya Russia, Kremlin, imetangaza habari ya kukamatwa watu 11, wakiwemo wanne waliohusika moja kwa moja katika shambulio hilo la mjini Moscow la siku ya Ijumaa, na kuua makumi ya watu.

Idara ya Usalama ya Russia imesema kwamba, washukiwa wa shambulio hilo walipanga kuvuka mpaka na walikuwa wakiwasiliana na watu wengine upande wa Ukraine.

Shirika la habari la TASS limemnukuu Katibu wa Baraza la Usalama la Russia, Nikolai Patrushev, ambaye ni mshirika mashuhuri wa Rais Vladimir Putin, akisema jana Jumamosi kwamba waliohusika na shambulio hilo wote wataadhibiwa.

342/