Main Title

source : Parstoday
Jumapili

24 Machi 2024

14:22:35
1446528

Idadi ya waliofariki katika shambulio la Moscow yapindukia 130, ISIS-K yadai kuhusika

Vyombo vya sheria na usalama vya Russia vimesema idadi ya watu waliouawa katika shambulio la kigaidi la siku ya Ijumaa kwenye ukumbi wa tamasha la muziki wa Crocus City Hall nje kidogo ya jiji la Moscow imepindukia watu 130.

Kwa mujibu wa Idara ya Usalama wa Ndani ya Russia FSB, wakati washukiwa 11 wakiwemo watu wanne wanaodaiwa kutekeleza mauaji hayo wakiwa wametiwa nguvuni, watu wasiopungua 133 wamethibitishwa kufariki hadi sasa na wengine zaidi ya 150 wamejeruhiwa.

Maelezo kuhusu utambulisho wa washukiwa na mazingira ya jinsi shambulio hilo lilivyofanywa yanaendelea kutolewa. Kulingana na FSB, shambulio hilo lilipangwa kwa uangalifu likilenga kusababisha maafa makubwa ya roho za watu.

Taarifa ya idara ya usalama wa ndani ya Russia imebainisha kuwa, washukiwa hao wanne wakuu walikamatwa alfajiri ya kuamkia jana Jumamosi katika Mkoa wa Bryansk nchini Russia unaopakana na Ukraine wakijaribu kutorokea chini humo. Washukiwa wengine walitiwa nguvuni katika mkoa wa mji mkuu Moscow.Maafisa wa vyombo vya sheria vya Russia hawajatoa taarifa zozote kuhusu majina au utaifa wa watuhumiwa 11 wanaowashikilia, hata hivyo Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi hiyo imethibitisha tu kwamba hakuna hata mmoja kati ya washukiwa wakuu ambaye ana uraia wa Russia.

Baadhi ya vyombo vya habari vya Magharibi, ikiwemo Reuters na CNN, vimeripoti kuwa kundi la kigaidi la Dola la Kiislamu la Mkoa wa Khorasan ISIS-K lenye mfungamano na DAESH (ISIS) limedai kuhusika na shambulio hilo. Kundi hilo limesema shambulio hilo ni sehemu ya "vita vikali" vya ISIS dhidi ya nchi zinazopigana na Uislamu. Moscow haijatoa maoni yoyote kuhusu madai hayo.../


342/