Main Title

source : Parstoday
Jumapili

24 Machi 2024

14:23:22
1446529

Bajeti ya muda ya US yaidhinisha msaada wa kijeshi kwa Israel, yazuia ufadhili kwa UNRWA

Bunge la Marekani limepitisha pendekezo la bajeti ya muda ambayo imeidhinisha msaada mpya wa kijeshi kwa utawala wa Kizayuni wa Israel na kusitisha ufadhili kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) hadi Machi 2025.

Bajeti hiyo ya muda ya dola trilioni 1.2 ambayo imeshasainiwa na Rais wa Marekani Joe Biden haijatenga fungu lolote la msaada wa fedha kwa UNRWA kwa muda wa mwaka mzima huku kukiwa na wasiwasi mkubwa wa kuzuka baa la njaa katika Ukanda wa Ghaza. Shirika hilo la Umoja wa Mataifa lilipoteza mamilioni ya dola za msaada wa kimataifa kupitia kampeni iliyoongozwa na  Marekani ya kukatisha misaada hiyo kufuatia madai ya Israel kwamba baadhi ya wafanyakazi wa UNRWA katika Ukanda wa Ghaza walihusika katika mashambulizi ya Oktoba 7, 2023 yaliyoongozwa na Hamas dhidi ya utawala huo wa Kizayuni. Bajeti ya muda ya serikali ya Marekani iliyonusuru kusimama kwa shughuli za kifedha za serikali na ambayo imeungwa mkono na vyama vyote viwili vya Democrats na Republicans, imeendelea kudumisha utoaji misaada ya kijeshi kwa utawala wa Kizayuni unaoendesha vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Ghaza.

Bajeti hiyo ya muda imetenga dola bilioni 3.8 za msaada wa kijeshi kwa ajili ya Israel kutoka kwenye bajeti yote ya dola bilioni 886 za wizara ya ulinzi ya nchi hiyo Pentagon.

Fungu jengine la fedha lililotengwa kwenye bajeti hiyo ya muda ni dola bilioni 95, zikiwemo dola bilioni 60 kwa ajili ya Ukraine na dola bilioni 14 kwa ajili ya Israel.

Wakati huohuo, Seneta wa chama cha Democratic Chris Van Hollen ameandika katika mtandao wa X: "kama nilivyokwisha eleza mara kadhaa: mtu yeyote aliyehusika katika shambulio la 10/7 lazima awajibishwe. Ndio maana uchunguzi huru unachunguza tuhuma kama hizo dhidi ya wafanyikazi 14 kati ya elfu 13 wa UNRWA. Lakini hatupaswi kuwaadhibu watu milioni mbili wasio na hatia na wenye njaa kwa vitendo vya watu hao".

Bajeti hiyo ya muda iliyopitishwa na bunge la Marekani na kusainiwa na rais wa nchi hiyo inajumuisha fedha kwa ajili ya wizara ya mambo ya nje, usalama wa ndani, ulinzi, kazi na afya, huduma za kibinadamu, pamoja na fedha za operesheni za nje ya nchi, huduma za kifedha na bunge. Fungu jengine la fedha za matumizi kwa ajili ya sehemu iliyosalia ya serikali liliidhinishwa na Kongresi wiki mbili zilizopita.../

342/