Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

25 Machi 2024

14:20:06
1446747

Shahidi: Wanajeshi wa Israel wamewabaka wanawake wa Kipalestina kabla ya kuwaua katika Hospitali ya al-Shifa

Mwanamke wa Kipalestina amesimulia matukio ya kutisha baada ya wanajeshi wa Israel kuvamia Hospitali ya al-Shifa katika mji wa Gaza wiki iliyopita, na kusema kuwa wanajeshi wa utawala huo ghasibu wanawabaka wanawake wa Kipalestina kabla ya kuwaua.

Jamila Al-Hisi, shahidi ambaye alizingirwa katika jengo la Hospitali ya al Shifa na hatimaye kufanikiwa kutoroka, amesema kwamba wanawake wamekuwa wakibakwa, kuumizwa kwa njaa, kuteswa na kunyongwa bila ya kuhukumiwa, na kuongeza kuwa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu haifanyi lolote kuwasaidia Wapalestina.

Al-Hisi anaendelea kusimulia kwamba, wanajeshi wa Israel wamezilazimisha familia 65 kuondoka katika eneo la karibu Hospitali ya la Al-Shifa na kuchoma moto na kuua familia nzima. Amesema kuwa wanajeshi hao pia wamechoma jengo ambalo raia wa Palestina walikuwa wanajihifadhi ndani yake.

Akieleza kwa majonzi, Jamila Al Hisi anasema: "Hatuna hata maji kwa ajili ya kufuturu, na hatujui pa kwenda." Amesema watu waliohamishwa kwenye nyumba zao hawajapata chakula au maji kwa siku sita.Ametoa wito kwa Shirika la Msalaba Mwekundu kuwapatia maji watoto na wagonjwa wanaolazimishwa kunywa maji machafu na kula vyakula vilivyooza. Matukio haya yanakuja huku jeshi la Israel likiendelea kufanya mashambulizi ya anga na mizinga ndani na karibu na Hospitali ya al-Shifa kwa siku ya saba mfululizo. Jumatatu iliyopita, askari wa Israel walivamia Hospitali ya al-Shifa huko Gaza kwa kutumia vifaru na ndege zisizo na rubani, wakidai kuwa harakati ya Hamas inatumia kituo hicho "kuendesha na kuendeleza shughuli za kigaidi." Wizara ya Afya ya Gaza inasema takriban watu 3,000 walikuwa ndani ya Hospiitali ya al-Shifa walikokimbilia usalama na kwamba wale waliojaribu kuondoka walilengwa kwa risasi za askari vamizi na helikopta za Israel.

342/