Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

25 Machi 2024

14:24:30
1446753

Guterres akiri kashfa ya kimaadili ya utawala wa Kizayuni katika kuzuia misaada ya kibinadamu kuingia Gaza.

Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ametembelea kivuko cha Rafah (kati ya Ukanda wa Gaza na Misri), katika mwezi wa sita wa mauaji ya halaiki ya utawala wa Kizayuni huko Gaza, na kukitaja kitendo cha utawala huo wa Kizayuni cha kuzuia misaada ya kibinadamu kuingia Gaza kuwa ni "kashfa ya kimaadili".

Mwezi wa sita wa vita vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Gaza unakaribia kumalizika, miezi ambayo utawala huo katili umetekeleza mauaji ya kimbari dhidi ya wakaazi wa Gaza. Kwa mujibu wa Guterres, Tel Aviv inatekeleza siasa haramu na zisizo za kibinadamu za kuwaadhibu kwa pamoja Wapalestina, ambazo haziwezi kuhalalishwa kwa njia yoyote ile. 

Moja  ya siasa hizo za adhabu ya umati ni kuzuia misaada ya kibinadamu kuingia Gaza huku watu wa ukanda huo hasa watoto wakifa kwa njaa. Kwa msing huo, huku akibainisha kuwa wakati wa kutekelezwa usitishwaji vita wa harakati kwa sababu za kibinadamu umewadia, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema inasikitisha kuona kwamba malori yameegeshwa upande mmoja wa kivuko huku baa la njaa likishuhudiwa katika upande wa pili. Watoto, wanawake na wanaume wa Palestina waliokimbia makazi yao wanaendelea kushuhudia "jinamizi lisilo na mwisho". Guterres ameongeza kuwa, wakati umefika kwa Israel kuthibitisha nia yake ya kufikishwa misaada ya kibinadamu katika maeneo yote ya Gaza na kuachiwa huru mateka wote mara moja.Suala jingine ni kuwa, ziara ya Guterres imefanyika katika hali ambayo, licha ya maombi ya kimataifa ya kutaka kuzuiwa mashambulizi ya Israel dhidi ya Rafah, utawala wa Tel Aviv unatishia kuanzisha operesheni ya kijeshi ya nchi kavu katika mji wa Rafah, kusini mwa Gaza, karibu na mpaka na Misri kwa uungaji mkono wa Washington. Kuhusiana na hilo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameonya kuwa, kufanyika shambulio jingine kubwa huko Gaza kutawazidishia Wapalestina machungu yanayowakabili kwa sasa.

Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa mara kadhaa amekuwa akibainisha wazi misimamo wake kuhusu hali ya Gaza. Amekuwa akionya mara kwa mara kuhusu hali mbaya ya kibinadamu huko Gaza na kusisitiza kuwa hali kama hiyo haijawahi kushuhudiwa tena katika  historia. Moja ya hatua muhimu alizozichukua Guterres kuhusu Gaza ni kutumia kifungo cha 99 cha Hati ya Umoja wa Mataifa, ambacho kilikuwa hakijatumika kwa miongo kadhaa. Kifungu hicho kinampa mamlaka Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuangazia masuala yanayotishia amani na usalama wa kimataifa.Licha ya msimamo huo thabiti na wa kufana wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, lakini taasisi hiyo ya kimataifa imeshindwa kusimamisha mauaji ya kimbari huko Gaza. Suala hilo linatokana na hatua ya nchi tatu za Magharibi yaani Marekani, Uingereza na Ufaransa ambazo ni wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama, ya kupinga azimio lolote la kusitisha vita huko Gaza. Kivitendo nchi hizo zimeufanya Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama kuwa chombo chao muhimu cha kutetea maslahi haramu ya Wazayuni na kwa msingi huo zinashiriki kikamilifu katika kashfa ya kimaadili ya utawala wa Kizayuni.

342/