Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

25 Machi 2024

14:25:06
1446754

Matteo Salvini: Macron mpiga ngoma ya vita ni "hatari" kwa Ulaya

Naibu Waziri Mkuu wa Italia, Matteo Salvini, amesema Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, ni "mchochezi wa vita" na ni "hatari" kwa Ulaya kwa kuendelea kushikamana na msimamo wake wa kutuma wanajeshi wa nchi kavu wa nchi za Magharibi huko Ukraine.

Matamshi haya ya Salvini yametolewa wakati wa mkutano wa Roma wa viongozi wa mrengo wa kulia na wa kitaifa wa Ulaya kabla ya uchaguzi wa wabunge wa EU mwezi Juni mwaka huu.

Salvini ambaye chama chake cha siasa kali za mrengo wa kulia cha League ni mshirika katika serikali ya mseto ya Waziri Mkuu Giorgia Meloni, amesema kwamba pendekezo la Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron mwezi uliopita kwamba wanajeshi wa nchi kavu wa Magharibi wanaweza kutumwa Ukraine lilikuwa hatari sana kupita kiasi na halina mlingano.

"Nadhani Rais Macron, kwa maneno yake, anawakilisha hatari kwa nchi yetu na bara letu," amesisitiza Naibu Waziri Mkuu wa Italia.

"Tatizo sio akina mama na baba, lakini ni wapenda vita kama Macron ambao wanazungumza juu ya vita kana kwamba hakuna tatizo lolote kwa sasa. Sitaki kuwaachia watoto wetu bara ambalo liko tayari kuingia katika Vita vya Tatu vya Dunia" amesisitiza Salvini.

Katika matamshi kama hayo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia, Antonio Tajani, pia alisema katikati ya mwezi huu wa Machi kwamba nchi yake haiungi mkono suala la kutumwa wanajeshi wa NATO nchini Ukraine, akionya kwamba hatua hiyo inaweza kuzusha Vita vya Tatu vya Dunia.Mwezi uliopita, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa alizungumzia waziwazi uwezekano wa kutuma wanajeshi wa Ulaya nchini Ukraine ili kupigana na Russia.

342/