Main Title

source : Parstoday
Jumatano

27 Machi 2024

13:40:40
1447195

Kuendelea kushambuliwa na kuzingirwa hospitali za Gaza na utawala wa Kizayuni

Licha ya wasiwasi mkubwa na maonyo ya mara kwa mara ya viongozi wa nchi mbalimbali na taasisi za kimataifa, utawala wa Kizayuni bado unaendelea kushambulia na kuzizingira hospitali za Gaza.

Tangu 7 Oktoba 2023 hadi leo hii, utawala wa Kizayuni sambamba na kutekeleza mauaji ya kimbari huko Gaza umekuwa ukitumia mbinu zisizo za kimaadili wala kibinadamu kufikia malengo yake haramu huko Gaza. Miongoni mwa mbinu hizo chafu ni pamoja na kuwaweka njaa watu wa Gaza, kushambulia hospitali na vituo vya matibabu, kuzuia kupewa matibabu  wagonjwa, kutisha na kuwanyanyasa madaktari na wauguzi wa eneo hilo.

Kuwaweka njaa raia hususan watoto wa Gaza kumesababisha matukio machungu ya watoto kupoteza maisha kutokana na njaa na kuwalazimisha kula chakula cha mifugo, jambo ambalo limetajwa na Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, kuwa kashfa ya maadili kwa utawala wa Kizayuni na vilevile jamii ya Kimataifa.

Kitendo cha kushambuliwa hospitali kilianza mwezi wa kwanza wa vita dhidi ya Gaza. Huku ukishambulia hospitali na kuvizingira vituo vya matibabu, utawala katili wa Kizayuni umeharibu kabisa vifaa vya matibabu, kuua shahidi idadi kubwa ya madaktari na wauguzi,  wagonjwa na wakati huo huo kuzuia idadi kubwa ya wagonjwa na wafanyakazi wa vituo vya afya katika hospitali hizo. Utawala huo haramu na katili unahalalisha vitendo vyake hivyo visivyo vya kibinadamu kwa kudai kwamba makamanda wa Hamas wamejificha kwenye mahandaki yaliyochimbwa chini ya hospitali hizo. Hata hivyo, madai hayo hayajathibitishwa na yanaendelea kusababisha kuongezeka idadi ya maafa ya kibinadamu huko Gaza.Katika kuendeleza jinai hizo dhidi ya hospitali na vituo vya matibabu, utawala wa Kizayuni tokea wiki moja iliyopita umezingira na kushambulia mara kadhaa Hospitali ya Al-Shifa iliyoko magharibi mwa mji wa Gaza. Tangu mwanzoni mwa juma lililopita, hospitali hiyo imekuwa katika mzingiro na mashambulizi ya kikatili ya jeshi vamizi la Isreal, na hadi sasa mamia ya wahudumu wa afya, wagonjwa na wakimbizi waliopata hifadhi ndani ya hospitali hiyo wameuawa shahidi au kujeruhiwa. Kwa muda wa wiki moja, watu waliozuiliwa katika Hospitali ya Al-Shifa na nyumba zinazoizunguka hawajakuwa na chakula wala maji. Kwa mujibu wa vyanzo vya habari, moja ya jinai za kutisha zinazofanywa na askari hao vamizi katika hospitali ya Al-Shifa ni kuwabaka wanawake wakiwemo wajawazito mbele ya familia zao na waume zao na kisha kuwaua shahidi. Hospitali ya al Amal iliyoko Khan Yunis ni kituo kingine cha matibabu ambacho kimezingirwa na jeshi la Kizayuni. Kwa mujibu wa vyanzo vya habari, jeshi vamizi bado linaendeleza mashambulizi yake ya makombora karibu na hospitali hiyo. Shirika la Hilali Nyekundu la Palestina limetangaza kukatika mawasiliano na wafanyakazi wake katika hospitali hiyo huko Khan Yunis na kwamba hakujakuwa na mawasiliano ya simu wala intaneti na wafanyakazi hao kwa siku 72 mfululizo. Kituo cha matibabu cha Al-Nasser huko Rafah ni moja ya vituo vingine vya matibabu vinavyozingirwa na kushambuliwa mara kwa mara na wavamizi wa Kizayuni. Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu imeripoti kwamba kwa mara nyingine hospitali za Amal, Nasser na al-Shifa zinakabiliwa na mashambulizi makali ya mara kwa mara. Utawala wa Kizayuni unaendeleza jinai hizo dhidi ya hospitali, vituo vya matibabu, wahudumu wa afya na wagonjwa wa Palestina, wakati ambapo kwa mujibu wa nyaraka na mikataba ya kimataifa, maeneo na wahudumu hao wote wanapaswa kuwa salama wakati wa vita. Pamoja na hayo yote, lakini madola ya Magharibi bado yanadai kuwa utawala wa Kizayuni una haki ya kujilinda na kutaka usilaaniwe kwa vyo vyote vile kutokana na mauaji na jinai za wazi unazotekeleza dhidi ya watu wasio na hatia.

342/