Main Title

source : Parstoday
Jumatano

27 Machi 2024

13:44:10
1447200

"Siku ya Quds imebakisha hai kadhia ya Palestina"

Mkuu wa Makao Makuu ya Intifadha na Siku ya Quds ya Iran amesema maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds yana umuhimu mkubwa katika kubakisha hai kadhia ya ukombozi wa Palestina.

Brigedia Jenerali Ramazan Sharif sambamba na kugusia umuhimu mkubwa wa Siku ya Quds, amesema kuwa, siku hiyo iliyotangazwa na Imam Khomeini MA, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hushuhudia maandamano ya pili kwa ukubwa hapa nchini, baada ya yale ya 22 Bahman (Februari 11) kila mwaka ya kuadhimisha Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979.

Aidha amekariri na kutilia mkazo kauli ya Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwamba, hakuna shaka utawala wa Kizayuni utaangamizwa na muqawama na uthubutu wa wananchi wa Palestina ambao ndio wamiliki halisi wa ardhi ya Palestina.

Brigedia Jenerali Ramazan Sharif vilevile amewataka Waislamu kote duniani hususan taifa la Iran kushiriki kwa wingi katika maandamano ya Siku ya Quds, ambayo huadhimishwa katika Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, ili kuonesha uwezo na umoja wao mbele ya maadui.Kadhalika Mkuu wa Makao Makuu ya Intifadha na Siku ya Quds amewakosoa vikali 'wasaliti' wa umma wa Kiislamu na ulimwengu wa Kiarabu ambao wanausaidia na kuuunga mkono utawala wa Kizayuni katika vita vyake dhidi ya Ukanda wa Gaza kwa miezi sita sasa. Amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea kuliunga mkono kwa hali na mali taifa la Palestina, na pia kushirikiana na nchi zinazojitenga na utawala wa Kizayuni wa Israel.

342/