Main Title

source : Parstoday
Jumapili

31 Machi 2024

17:41:27
1448035

Maadhimisho ya YaumuLlah, Siku ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

YaumuLlah ya tarehe 12 Farvardin mwaka 1358 Hijria Shamsia (iliyosadifiana na Aprili Mosi, 1979), yenye maana ya Siku ya Mwenyezi Mungu, si siku rasmi tu katika kalenda ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, bali ni siku kubwa pia kwa wanyonge duniani na kwa harakati za ukombozi pamoja na mataifa yanayopambana na dhulma, uistikbari na ukoloni.

Baada ya kupita mwezi mmoja tu na ushee tokea Mapinduzi ya Kiislamu yalipopata ushindi, wananchi Waislamu wa Iran walishiriki katika kura ya maoni ya kihistoria na kuupigia kura za "ndiyo" uamuzi wa kuasisi Mfumo mtakatifu wa Jamhuri ya Kiislamu katika ardhi na jiografia ya Iran na kuyabadilisha Mapinduzi ya Kiislamu kuwa Mfumo wa Kiislamu na kupiga hatua kubwa katika kuliinua jina la Iran duniani.

Tarehe 12 Farvardin kila mwaka inakumbusha kufanyika moja ya kura za maoni kubwa na muhimu zaidi katika historia ya mwanadamu, ambapo wananchi wanamapinduzi wa Iran waliunga mkono kwa takribani 99% kuasisiwa kwa Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu nchini Iran.

Kwa hivyo tarehe 12 Farvardin, Siku ya Jamhuri ya Kiislamu, ni moja ya siku zenye kumbukumbu kubwa zaidi katika siku za Mapinduzi ya Kiislamu; na si kwa watu wa Iran pekee, bali kwa watu wote waliokomboka kifikra.

Imam Khomeini (MA), Muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliielezea Farvardin 12 kwa kusema: "siku hii ni siku ya kwanza ya Utawala wa Kiislamu na ni YaumuLlah, na ni siku ambayo wananchi wa Iran walizitekeleza aya za Mwenyezi Mungu na kuuhuisha Uislamu".

Kwa hivyo, YaumuLlah ya tarehe 12 Farvardin, ni moja ya siku muhimu zaidi iliyopambanua kipindi muhimu katika historia ya mwanadamu, na si kwa Iran pekee bali pia kwa wapenzi wa Mapinduzi ya Kiislamu; na siku hii, ni dhihirisho la kuthibiti matakwa ya wananchi ya kujiamulia hatima na mustakabali wao chini ya uongozi wa Imam Khomeini (MA) na kukataa kila aina ya ubeberu wa maajinabi dhidi ya Iran.Ali Sharifinia, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anaeleza yafuatayo kuhusiana na hili: "Farvardin 12 inakumbusha siku ya kuushinda ukoloni na uistikbari wa zama. Siku hii ni siku ya utukufu na ya kujivunia kwa watu waliopambana na kuushinda utawala wa kidikteta kwa mikono mitupu huku wakiwa chini ya uongozi imara na thabiti wa shakhsia mweledi na mwenye busara. Na bila kupoteza muda, wakashiriki kwenye kura ya maoni ya kihistoria na isiyowahi kushuhudiwa, na kuidhinisha takwa lao la kuasisi Mfumo mtakatifu wa Kiislamu”.

Mfumo wa Kiislamu uliotokana na matakwa ya wananchi na kuasisiwa kwa jina la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ulianzishwa na kurasimishwa kwa ridhaa ya 98.2% ya kura za wananchi.

Ukweli ni kwamba, kura ya maoni ya tarehe 12 Farvardin na Siku ya Jamhuri ya Kiislamu ilikuwa matunda na matokeo ya miaka mingi ya mapambano ya wananchi wenye imani ya kweli ya dini wa Iran, ambao walitaka wajitawale kisiasa na kuwa huru kwa kujivua pingu na minyororo ya kikoloni na kiistikbari. Jamhuri ya Kiislamu ni mmea mchanga uliochipua, lakini uliazimia kwa dhati kuvuka mipaka yake ya kijiografia hatua kwa hatua, licha ya kuandamwa na njama za mtawalia za maadui; na ukaweza kufikia hatua ya kugeuka kuwa tumaini la mataifa yote yanayotaka kuzikata pingu za mfumo wa ubeberu hususan wa Marekani na Uingereza na kuwa na mamlaka ya kujiamulia mustakabali wao. Kuendelea kwa harakati za kupinga ubeberu na kuasisiwa na kuimarika kambi ya Muqawama ni matokeo ya kupanuka zaidi na zaidi wigo wa utamaduni wa Mapinduzi ya Kiislamu ulimwenguni kote.Kwa hiyo, kwa mukhtasari tunaweza kusema kwamba, kwa upande wa ndani ya Iran, tarehe 12 Farvardin ni siku ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, siku ya kubadilishwa mfumo wa kifalme kuwa Jamhuri ya Kiislamu na kupatikana mamlaka ya kujitawala kisiasa. Na katika uga wa kikanda na kimataifa, ni siku inayotuma ujumbe wa wazi kwa watu wote wanaopigania uhuru na kujitawala kwamba inawezekana kuushinda kwa mikono mitupu mfumo tawala wa kidhalimu na kibeberu.

Hivi sasa wananchi hao wa Iran wanazungumza kwa fakhari kubwa pia juu ya Mhimili wa Muqawama, ambao ni zao la Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran, unaopambana na uvamizi na ukaliaji ardhi kwa mabavu wa Wazayuni. Ijapokuwa Mapinduzi ya Kiislamu yalikamilika rasmi ndani ya mipaka ya kijiografia ya Iran kwa kura ya maoni ya tarehe 12 Farvardin, lakini baada ya kupita zaidi ya miongo minne, yamegeuka kuwa mti imara ambao umesaidia kupatikana haki za wanyonge duniani kwa kuleta mlingano wa nguvu; na hivi sasa hayajabaki kuwa mhimili wa nguvu tu, bali yameshakuwa pia mhimili wa kuleta mlingano katika upeo wa kikanda na kimataifa…/


342/