Main Title

source : Parstoday
Jumapili

31 Machi 2024

17:41:58
1448036

Jihad Islami: Wapalestina hawangeweza kusimama dhidi ya Israel bila ya kuungwa mkono na Iran

Kiongozi mkuu wa Harakati ya Jihad Islami ya Palestina ametangaza bayana kuwa watu wa Palestina hawangeweza kusimama dhidi ya utawala haramu wa Israel kama kusingekuwa na uungaji mkono kamili wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihad Islami  ya Palestina Ziyad al-Nakhaleh aliyasema hayo jana Jumamosi katika mkutano na waandishi wa habari akiwa na Hossein Amir-Abdollahian Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran mjini Tehran.

Amepongeza nafasi muhimu ya Iran katika kuunga mkono muqawama au mapambano ya wananchi wa Palestina tangu utawala wa Israel ulipoanzisha vita vya mauaji ya halaiki dhidi ya watu wa Gaza mapema Oktoba 2023.

Amebaini kuwa diplomasia hai ya Iran imechukua nafasi kubwa katika kufafanua msimamo wa harakati za kupigania ukombozi wa Palestina.

Kiongozi huyo wa Jihad Islami amesisitiza kuwa wananchi wa Palestina watapata ushindi wa mwisho katika vita vyao dhidi ya Israel na kusema kuwa kusimama kidete Wapalestina kutakuwa kigezo cha kuigwa na watu wote wa dunia.

Nakhaleh ameongeza kuwa, Iran imelipa gharama ya uungaji mkono wake wa mara kwa mara kwa mapambano ya wananchi wa Palestina na utetezi wake wa haki za Wapalestina ambapo ameashiria mfano vikwazo vingi ambavyo Iran imewekewa na madola ya Magharibi.Amemshukuru Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Seyyed Ali Khamenei na viongozi na taifa la Iran kwa kuiunga mkono Palestina.

Vita vya mauaji ya halaiki vya Israel vinavyoungwa mkono na Marekani vilianza baada ya Hamas kutekeleza operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa mnamo Oktoba 7, 2023, dhidi utawala huo katili ikiwa ni mojawapo ya hatua za kulipiza kisasi kwa ukatili dhidi ya watu wa Palestina.

Takriban miezi sita baada ya vita kuanza, utawala ghasibu wa Israel umeshindwa kufikia malengo yake ya eti "kuiangamiza Hamas" na kuwaokoa mateka Wazayuni. Hadi sasa utawala haramu wa Israel umeua shahidi Wapalestina wasiopungua 32,705 wengi wao wakiwa wanawake na watoto na kuwajeruhi wengine zaidi ya 75,190.



342/