Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

1 Aprili 2024

14:13:18
1448208

Makundi ya ukombozi ya Palestina: Hatutaruhusu jeshi lolote la kimataifa au la Kiarabu kuingia Gaza

Makundi ya ukombozi ya Wapalestina yametangaza kuwa jeshi lolote la kimataifa au la Kiarabu litakaloingia katika Ukanda wa Gaza halikubaliki na litatambuliwa kuwa ni jeshi vamizi.

Hayo yamesemwa katika taarifa ya Kamati ya Ufuatiliaji ya Harakati za Kitaifa na Kiislamu, ambayo inajumuisha makundi mengi ya ukombozi ya Palestina. Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imechapisha taarifa hiyo kwenye majukwaa yake ya mitandao ya kijamii, kwa mnasaba wa kuadhimisha miaka 48 ya Siku ya Ardhi ya Palestina.

Makundi hayo yamesema, "Kauli za viongozi wa utawala ghasibu kuhusu kuundwa jeshi la kimataifa au la Kiarabu kwa ajili ya Ukanda wa Gaza ni ndoto na sarabi, na jeshi lolote litakaloingia katika Ukanda wa Gaza ni vamizi na haikubaliki, na litashughulikiwa kwa mujibu wa msimamo huo."

Taarifa ya makundi ya mapambano ya ukombozi ya Palestina imeongeza kuwa: "Tunathamini msimamo wa nchi za Kiarabu ambazo zimekataa kushiriki na kushirikiana na pendekezo la viongozi wa utawala vamizi wa Israel kuhusu kuundwa kwa kikosi hicho."

Makundi hayo yamesisitiza kuwa, kusimamia masuala ya Palestina ni "suala la ndani la taifa la Palestina ambalo hatutamruhusu mtu yeyote kuliingilia, na majaribio yote ya kuunda tawala mbadala zinazokwenda kinyume na matakwa ya watu wa Palestina yatakufa kabla ya kuzaliwa.”Ijumaa iliyopita, vyombo vya habari vya Israel viliripoti kwamba Waziri wa Ulinzi wa utawala huo, Yoav Galant, alimfahamisha Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kuhusu maendeleo katika mazungumzo na Marekani yanayohusiana na pendekezo la kupelekwa kikosi cha kimataifa katika eneo la Ukanda wa Gaza. Televisheni ya Israel imeripoti kwamba, Gallant alifanya mazungumzo na maafisa wa serikali ya Marekani, wakati wa ziara yake huko Washington siku chache zilizopita, kuhusu kuundwa kikosi cha kimataifa na kukipeleka Gaza kusimamia usalama wa eneo hilo, badala ya Wapalestina wenyewe. Haukujulikana iwapo kikosi hicho kitajumuisha wanajeshi wa Marekani au la.

342/