Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amefanya mazungumzo ya simu na Sameh Hassan Shoukry, waziri mwenzake wa mambo ya nje wa Misri na kujadiliana naye njia za kuhakikisha utawala wa Kizayuni hauuvamii mji wa Rafah ambao sehemu kubwa ya wananchi wa Ghaza wamekimbilia huko.
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Misri wamepinga njama zote za utawala wa Kizayuni za kutaka kuwahamisha kwa nguvu Wapalestina kwenye Ukanda wa Ghaza na kuhimiza kuchukuliwa hatua za kimataifa za kuzuia jinai zaidi za Israel huko kusini mwa Ghaza.
Mawaziri hao wameelezea pia kuridhishwa kwao na juhudi zilizofanywa na pande hizi mbili katika miezi ya hivi karibuni kwa ajili ya kuimarisha uhusiano baina yao na kuelezea matumaini yao kuwa viongozi wa kisiasa wa nchi hizi mbili za Kiislamu watachukua hatua kubwa zaidi ya kurejesha uhusiano baina ya Tehran na Cairo ambao kwa hakika ni muhimu kwa ulimwengu mzima wa Kiislamu na kwa utulivu na amani ya eneo hili zima.
342/