Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

1 Aprili 2024

14:19:39
1448213

Msaada mpya wa silaha wa Marekani kwa Israel wa kufanyia mauaji makubwa zaidi ya kimbari ya Wapalestina

Sambamba na juhudi zinazofanywa kimataifa kwa lengo la kusimamisha mauaji ya kimbari ya Wapalestina yanayofanywa na utawala wa Kizayuni; na mashinikizo yanayotolewa kwa utawala huo uhakikishe unaruhusu kuingizwa misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Ghaza, duru za habari za Marekani zimeripoti kuwa serikali ya Washington imeidhinisha kupatiwa Israel shehena mpya ya silaha za kisasa ili kuweza kuua idadi kubwa zaidi ya Wapalestina.

Wakati serikali ya Marekani inadai eti inafanya juu chini ili vita visimamishwe huko Ghaza na pande mbili kubadilishana mateka, ingali inaendelea kuuunga mkono na kuusaidia kifedha, kijeshi na kisiasa utawala dhalimu wa Kizayuni; na kwa kufanya hivyo kuhusika moja kwa moja katika jinai na mauaji ya kimbari unayofanya utawala huo dhidi ya wananchi wa Palestina. Kuhusiana na suala hilo, gazeti la Washington Post limefichua katika toleo lake la hivi karibuni kwamba, serikali ya Marekani imeafiki kuipatia Israel mabomu na ndege za kivita za kisasa ili kufanyia mauaji ya kimbari na ya halaiki dhidi ya Wapalestina wa Ghaza. Gazeti hilo limewanukuu maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na ya Ulinzi ya Pentagon na kuandika kuwa, wizara ya mambo ya nje imetoa kibali cha kupelekwa Israel ndege za kivita za kisasa 25 aina ya F-35A na mabomu 1,800 aina ya MK 84. Ripoti zilizowahi kutolewa huko nyuma zilionyesha kuwa kutumia Israel mabomu ya MK 84 na MK 82 kilikuwa ndio chanzo kikuu cha kutokea maafa makubwa ya vifo vingi vya raia katika Ukanda wa Ghaza.Duru za Kizayuni na za Marekani zimekiri kuwa, tangu yalipoanza mashambulio ya kinyama ya Wazayuni katika Ukanda wa Ghaza mnamo Oktoba 7, 2023, Washington imetuma zaidi ya ndege 230 za mizigo na meli 30 zilizobeba shehena za silaha kuupelekea utawala haramu wa Kizayuni. Ikumbukwe kuwa shehena hizo za silaha zimepelekwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu katika hali ambayo wiki iliyopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha kwa wingi mkubwa wa kura azimio la kuitaka Israel isitishe mara moja mashambulizi ya kinyama dhidi ya Ghaza na kuruhusu kuingizwa misaada katika eneo hilo bila kizuizi chochote. Uamuzi wa Washington wa kuipelekea silaha Israel umefanywa pia wakati waungaji mkono wa Palestina wamekuwa wakifanya maandamano katika majimbo mbalimbali ya Marekani hususan San Francisco, ambapo mbali na kupinga hatua yoyote inayoweza kuchukuliwa na Washington ya kuipelekea silaha Israel, wamesisitiza kwamba kufanya hivyo kutakuwa sawa na kushiriki nchi yao dhahir shahir katika mauaji ya kimbari ya Wapalestina. Siku ya Ijumaa, Seneta Bernie Sanders, alikosoa vikali uamuzi wa serikali ya Marekani wa kuipelekea silaha zaidi Israel na akasema, Marekani haiwezi kwa upande mmoja kudai kwamba inataka vita visimamishwe, na kwa upande mwingine kuafiki kuipatia Israel silaha za maangamizi; na kwamba hiyo ni sera chafu na ovu na yenye mgongano. Awamu mpya ya uungaji mkono wa silaha wa Marekani kwa Israel inashuhudiwa wakati siku hizi Washington inasikika ikidai kuwa, inatiwa wasiwasi na kushadidi mashambulizi ya Israel kwenye eneo la kusini ya Ghaza la Rafah, mahali walipokusanyika ili kutafuta hifadhi Wapalestina wapatao milioni moja na laki tatu. Katika hali hiyo, si siri tena kwamba kitendo cha serikali ya Joe Biden cha kutenga mabilioni ya dola za msaada wa kijeshi kwa Israel, ni ithibati ya wazi kabisa ya kuamua kuiunga mkono bila kificho Israel katika ufanyaji jinai kubwa zaidi dhidi ya binadamu.Marekani inaendelea kuipelekea misaada ya silaha Israel wakati maelfu ya wanawake na watoto wa Kipalestina wameshauawa shahidi katika mashambulizi ya kinyama yaliyofanywa na jeshi la utawala huo ghasibu huko Ghaza; ambapo kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Palestina, idadi ya Mashahidi wa mashambulio hayo yaliyoanza Oktoba 7, 2023 dhidi ya Ghaza inakaribia watu elfu 33 huku majeruhi wakikadiriwa kufikia watu elfu 75, mbali na zaidi ya 90% ya vifaa vya miundombinu vilivyoteketezwa ikiwa ni pamoja na vituo vya utoaji huduma za tiba vya eneo hilo lililowekewa mzingiro.Kuafiki kwenye maana maalumu kwa Marekani kuupatia utawala wa Kizayuni wa Israel shehena mpya ya silaha angamizi katika kipindi hiki hasasi na nyeti kunafanyika katika hali ambayo siku ya Ijumaa, Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ ilitoa indhari kwamba hali ya kibinadamu inazidi kuwa mbaya huko Ghaza na kuutaka utawala wa Kizayuni na waungaji mkono wake wasimamishe vita na kuchukua hatua zinazohitajika kuhakikisha misaada ya kibinadamu inawafikia haraka Wapalestina wa eneo hilo. Katika wito unaofanana na huo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wiki iliyopita lilipitisha azimio, ambalo mbali na kusisitiza kusitishwa mara moja mashambulizi ya Israel dhidi ya Ghaza, liliutaka utawala huo uondoe haraka vizuizi vinavyokwamisha upelekaji misaada ya kibinadamu kwa Wapalestina wa eneo hilo lililozingirwa.

Juhudi za asasi za kimataifa za kusimamisha jinai za utawala wa Kizayuni huko Ghaza zinafanyika huku Wazayuni wakiendeleza jinai hizo kwa uungaji mkono wa Marekani; na hivi sasa wanajiandaa kuzusha balaa na maafa mengine makubwa na ya kutisha katika mji wa mpakani wa Rafah kusini mwa Ukanda wa Ghaza.

Baada ya Wapalestina wapatao milioni moja na nusu wanaoishi kwenye maeneo tofauti ya Ghaza kulazimika kuyahama makazi yao na kukimbilia kwenye mji wa mpakani wa Rafah, hivi sasa utawala wa Kizayuni unadai kuwa unapanga kuushambulia kijeshi mji huo ili kuviangamiza vikosi vya Hamas vilivyoko katika eneo hilo.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu na hasa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameonya kuwa iwapo Rafah itashambuliwa, dunia itashuhudia mauaji makubwa zaidi ya kimbari ya Wapalestina. Katika hali hiyo, Marekani na Uingereza, zikiwa ni waungaji mkono wakuu wa jinai za Israel, badala ya kufanya juhudi za kusimamisha vita na mauaji ya Wapalestina, zinawapelekea silaha Wazayuni ili kuonyesha waziwazi uungaji mkono wao kwa mauaji ya kimbari yanayofanywa huko Ghaza. 

Kuunga mkono jinai za Wazayuni kunadhihirisha vipimo vya kiundumakuwili vinavyotumiwa na Wamagharibi katika kadhia ya Palestina; na ni kielelezo cha nyuso mbili tofauti wanazoonyesha katika uga wa haki za binadamu. Lakini pamoja na mashinikizo yote hayo, bila shaka kipindi hiki kigumu na cha mateso kinachowakabili Wapalestina na eneo hili kitapita, lakini historia itaandika na kuweka rekodi juu ya namna kila nchi na jumuiya za kimataifa zilivyochukua msimamo kuhusiana na mauaji ya wazi ya kimbari yaliyofanywa na utawala wa kinyama wa Israel dhidi ya Wapalestina madhulumu wa Ukanda wa Ghaza.../


342/