Main Title

source : Parstoday
Jumanne

2 Aprili 2024

14:37:11
1448519

Baada ya kufanya unyama mkubwa kwa majuma 2, jeshi la Israel laondoka Hospitali ya Al-Shifa

Jeshi la utawala haramu wa Kizayuni wa Israel limeondoka ndani ya Hospitali ya Al-Shifa na maeneo ya jirani magharibi mwa Mji wa Ghaza mapema jana Jumatatu na kuacha majeruhi wengi na uharibifu mkubwa katika hospitali hiyo na viunga vyake.

Kwa mujibu wa mashuhuda, jeshi la askari katili wa Kizayuni limejiondoa kikamilifu ndani ya hospitali hiyo na vitongoji vinavyoizunguka kuelekea maeneo ya kusini mwa kitongoji cha Tel al-Hawa, kusini magharibi mwa mji wa Ghaza. Mashuhuda hao wameongeza kuwa, katika muda wa majuma mawili wa kuivamia na kuikalia hospitali ya Al-Shifa, vikosi vya jeshi la Kizayuni vilichoma moto majengo yote katika hospitali hiyo na kupelekea kusitishwa utoaji huduma. Imeelezwa pia kwamba, jeshi la Israel limeharibu jengo la upasuaji maalumu na kuchoma moto jengo kuu la mapokezi na huduma za dharura. Vilevile askari katili wa utawala wa Kizayuni wamechoma moto majengo ya wodi za figo na wajawazito, mafriji ya kuhifadhia maiti, na vifaa vya matibabu ya kansa na majeraha ya kuungua, mbali na kubomoa jengo la kliniki ya wagonjwa wa nje.Kulingana na duru za tiba za Palestina, hospitali hiyo kwa sasa haitumiki kabisa kutokana na jeshi la Kizayuni kuharibu vifaa vyote vya matibabu katika vyumba vya wagonjwa, vyumba vya upasuaji na vyumba vya wagonjwa mahututi.

 Mashuhuda wameripoti kuwa, miili mingi iliyotawanyika imepatikana katika hospitali hiyo na katika mitaa inayoizunguka. Wameeleza pia kwamba askari wa jeshi la utawala haramu wa Israel wamebomoa eneo la makaburi ya muda lililoanzishwa na Wapalestina katika kituo hicho na kufukua maiti kwenye makaburi hayo na kuzitawanya katika maeneo mbalimbali ya hospitali hiyo ya Al-Shifa. Aidha wamebainisha kuwa wanajeshi wa Israel wamechoma moto na kubomoa nyumba nyingi na majengo ya makazi karibu na hospitali hiyo. Mnamo Machi 18, jeshi katili la utawala dhalimu wa Israel lilivamia Hospitali ya Al-Shifa, kituo kikubwa zaidi cha matibabu katika Ukanda wa Ghaza ambacho kinahifadhi maelfu ya wagonjwa na watu waliolazimika kuyahama makazi yao.../


342/