Katika shambulio la makombora lililofanywa jana na utawala wa Kizayuni kutokea eneo la Golan unalolikalia kwa mabavu na kulenga ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus, Jenerali Mohammad Reza Zahedi na Jenerali Mohammad Hadi Haj Rahimi pamoja na watu wengine watano waliokuwa pamoja nao waliuawa shahidi.Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Iran Press, Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imelaani vikali hujuma ya utawala wa Kizayuni dhidi ya jengo la ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus na kuitaka Israel iache vitendo vyake visivyokubalika katika eneo.Mumtaz Zahra, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan amelaani vikali shambulio la kigaidi la utawala wa Kizayuni katika ubalozi mdogo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Damascus na akalitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lichukue hatua ya kukomesha chokochoko za Israel katika eneo na hatua zake zilizo kinyume cha sheria za kushambulia majirani zake na kulenga vituo vya kidiplomasia vya kigeni. Taarifa ya kulaani shambulio la kigaidi la utawala wa Kizayuni dhidi ya ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus imetolewa pia na Wizara ya Mambo ya Nje ya Oman ambayo imelielezea shambulio hilo kuwa ni ukiukaji wa mamlaka ya kujitawala Syria na sheria zote za ulinzi wa balozi za kidiplomasia.
342/