Main Title

source : Parstoday
Jumanne

2 Aprili 2024

14:40:49
1448528

Iran: Uchunguzi wa kimataifa ufanyike kuhusu jinai ilizofanya Israel katika Hospitali ya Al-Shifa

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitizia ulazima wa kufanyika uchunguzi wa kimataifa kuhusiana na uharibifu, utesaji na mauaji yaliyofanywa na jeshi la Kizayuni katika Hospitali ya Al-Shifa huko Ukanda wa Ghaza.

Ofisi ya Habari ya Serikali ya Palestina katika Ukanda wa Ghaza imetangaza kuwa jeshi la Israel limefanya jinai za kubomoa na kuchoma moto nyumba 1,500 karibu na Hospitali ya Al-Shifa katika Jiji la Gaza. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wanajeshi wa Kizayuni wameua zaidi ya Wapalestina 400 katika mashambulizi yao dhidi ya hospitali ya Shafa katika siku chache zilizopita. Kuhusiana na suala hilo na kwa mujibu wa IRNA, Nasser Kan'ani, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, ameandika kwenye ukurasa wake binafsi wa mtandao wa intaneti kwamba: "mikanda ya video iliyoonyeshwa kutoka Hospitali ya Al-Shifa huko Ghaza baada ya mzingiro wa wiki mbili wa jeshi la Kizayuni, taarifa za mashuhuda waliokuwa kwenye eneo hilo na ripoti za mikanda ya video na za habari kuhusu ukubwa wa uharibifu uliofanywa, utesaji, mauaji na idadi ya Wapalestina waliotiwa nguvuni katika hospitali hii ni ya kutisha na ya kushtusha".Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran amesisitiza kuwa, kuna udharura wa haraka wa kufanyika uchunguzi wa kimataifa kuhusiana na jinai hizo na akahoji: "je, jumuiya na taasisi za kimataifa zitatekeleza wajibu wao? Je, wanaojulikana kwa kujinadi kuwa watetezi wa haki za binadamu wataunga mkono kufanyika uchunguzi wa kimataifa kuhusu ukubwa wa uhalifu huu wa wazi wa kivita au mwenendo uliozoeleka wa kufanya upendeleo na ubaguzi kuhusiana na haki za binadamu utaendelezwa?"

 Itakumbukwa kuwa, tangu tarehe 7 Oktoba 2023 na kwa uungaji mkono kamili wa nchi za Magharibi, utawala wa Kizayuni umekuwa ukifanya mauaji makubwa ya kimbari katika Ukanda wa Ghaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan dhidi ya wananchi wasio na ulinzi na madhulumu wa Palestina; na kimya kilichoonyeshwa na jamii ya kimataifa na taasisi za haki za binadamu kwa jinai za Israel zimepelekea kuendelezwa mauaji ya wanawake na watoto wa Kipalestina yanayofanywa na utawala huo wa haramu. Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Palestina, idadi ya waliouawa shahidi katika mashambulizi ya Israel kwenye Ukanda wa Ghaza tangu Oktoba 7, 2023 hadi sasa imefikia watu 32,782.../


342/