Main Title

source : Parstoday
Jumanne

2 Aprili 2024

14:41:18
1448529

Naibu Katibu Mkuu wa UN: Jaribio la kuitenga UNRWA lazima likome

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na uratibu wa misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura Martin Griffiths amesema shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA ni uti wa mgongo wa operesheni za kibinadamu Ghaza, hivyo jaribio la kulitenga shirika hilo lazima likome.

Griffiths ametoa kauli hiyo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X akisistiza kuwa juhudi zozote za kusambaza misaada ya kibindamu kwenye Ukanda wa Ghaza bila kupitia shirika la UNRWA haziwezi kufanikiwa na watu zaidi ya milioni mbili wanaitegemea UNRWA ili kuendelea kuishi. 

Ameendelea kusema kwamba "hadi sasa hakuna shirika lingine lolote lenye uwezo wa kufika kila kona ya Ghaza, na lenye uzowefu na imani ya jamii ya kutekeleza majukumu yake kama lilivyo shirika la UNRWA".

Wakati huohuo shirika la UNRWA limeonya kwamba mashambulizi ya jeshi la utawala wa Kizayuni Israel yaliendelea tena usiku wa kuamkia jana huko Ghaza Kaskazini, Khan Younis na Rafah ambako watu milioni moja na laki mbili wanapata hifadhi na kusababisha vifo zaidi.

Hayo yanaripotiwa huku Shirika la Afya Duniani WHO likisema, wakati timu yake ikiwa katika operesheni ya kibinadamu katika hospitali ya Al-Aqsa siku ya Jumapili maeneo ya hospitali hiyo yaliandamwa na shambulio la anga lililoua watu wanne na kujeruhi wengine 17.

Nalo Shirika la Mpango wa Chakula Duniani WFP limetangaza kuwa, linajitahidi kwa kila hali kutoa msaada wa chakula unaohitajika sana kwa watu karibu milioni moja na nusu huko Ghaza lakini msaada huo hautoshi na bila usitishaji vita hawawezi kumfikia kila mtu na hivyo kufanya maisha ya watu wengi yaendelee kuwa hatarini.../

342/