Main Title

source : Parstoday
Jumanne

2 Aprili 2024

14:42:36
1448532

Mbunge wa Marekani ataka kadhia ya Ghaza imalizwe kama zilivyofanyiwa Hiroshima na Nagasaki

Tim Walberg, Mbunge wa jimbo la Michigan Kusini nchini Marekani kwa tiketi ya chama cha Republican amelazimika kufuta kauli aliyotoa ya kutaka Ukanda wa Ghaza uliozingirwa, ambao ni makazi ya zaidi ya watu milioni mbili, ushughulikiwe kama ilivyofanyiwa miji ya Nagasaki na Hiroshima ya Japan ambayo ilishambuliwa na Marekani kwa mabomu ya nyuklia.

Walberg, ambaye aliwahi kuwa mchungaji wa Kanisa amefuta kauli yake hiyo baada ya kukosolewa vikali.Alipokuwa akihutubia mkutano wa watu wa jimbo lake wiki iliyopita, mbunge huyo aliulizwa kuhusu gati ya muda inayojengwa na Marekani karibu na Ghaza kwa ajili ya kupeleka misaada ya kibinadamu kwa watu wa eneo hilo, ambao Umoja wa Mataifa unasema wanakabiliwa na hatari kubwa ya baa la njaa. Katika jibu alilotoa, Walberg alisema: "hatupaswi kutumia hata senti moja kwa misaada ya kibinadamu". Akisema hayo kwenye video iliyowekwa mtandaoni Alkhamisi iliyopita, mbunge huyo aliongeza kuwa: "kila kitu kimalizwe haraka. Iwe vivyo hivyo kuhusiana na Ukraine".Akifafanua zaidi alisema: "inapasa iwe kama Hiroshima na Nagasaki," akimaanisha miji miwili pekee iliyoshambuliwa na Marekani kwa silaha za nyuklia, ambapo watu wapatao 226,000, wengi wao wakiwa raia, walipoteza maisha katika mashambulio hayo mnamo mwaka 1945.

 Lakini baada ya kukosolewa vikali, siku ya Jumapili Walberg alijaribu kufuta kauli yake katika ujumbe alioweka kwenye mtandao wa X akidai kuwa matamshi yake hayakuhaririwa kiinsafu. Mbunge huyo wa Kongresi ya Marekani ameongezea kwa kusema: "katika klipu iliyofupishwa, nilitumia sitiari kuwasilisha hitajio la Israel na Ukraine kushinda vita vyao haraka iwezekanavyo, bila kuwatia hatarini wanajeshi wa Marekani".../

342/