Main Title

source : Parstoday
Jumatano

3 Aprili 2024

20:45:13
1448811

Tofauti ya Siku ya Quds ya mwaka huu na ya miaka iliyopita

Siku ya Kimataifa ya Quds mwaka huu inakaribia katika hali ambayo siku hiyo itakuwa tofauti kabisa na siku nyingie za Quds za karne hii ya 21.

Siku ya Quds ni moja ya kumbukumbu za kudumu na za kufana zaidi za Imam Khomeini, Mwenyezi Mungu Amrehemu. Imam Khomeini, alibainisha wazi kabisa suala la kuangamizwa Israel na kutokomezwa kikamilifu utawala haramu na vamizi wa Kizayuni, na kutangaza Siku ya Quds kuwa moja ya mikakati ya kufikia lengo hilo. Siku ya Kimataifa ya Quds ni siku ambayo Waislamu katika nchi nyingi duniani hufanya maandamano ya kuunga mkono Palestina inayokaliwa kwa mabavu na Waazayuni.

Seyyed Hassan Nasrallah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon anasema: "Mwaka huu Siku ya Quds itaadhimishwa katika hali tofauti kabisa na ya miaka iliyopita, na ninawaomba watu wote sehemu zote hususan katika vitongoji vya kusini mwa Beirut, washiriki katika hafla maalum na kubwa itakayofanyika kwa ajili ya kusisitiza juu ya kujitolea kwetu kwa ajili ya Palestina."

Tofauti kubwa iliyopo kati ya Siku ya Quds ya mwaka huu na ya miaka iliyopita ni kwamba katika kipindi cha miezi 6 iliyopita utawala ghasibu na haramu wa Israel umekuwa ukitekeleza mauaji ya kizazi huko Gaza.

Wananchi wa Gaza wamekuwa wahanga wakuu wa vitendo vya kijinai vya utawala wa Kizayuni. Siku ya Quds mwaka huu inakaribia huku watoto wa Gaza wakikabiliwa na njaa na uhaba mkubwa wa chakula, ambapo Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa watu milioni 1.1 wa Gaza wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula. Watoto wa Gaza wanapoteza maisha kutokana na baa la njaa. Siku ya Quds itaadhimishwa Ijumaa huku Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akitangaza kuhuzunishwa kwake na yanayotokea Gaza.

Siku ya Quds mwaka huu inakaribia huku Jumuiya za kimataifa zikiwa zimeshindwa kukabiliana na jinai za Wazayuni. Licha ya kuwa mataifa mengi duniani yakiwemo Marekani, Uingereza, Ujerumani na Ufaransa yanalaani jinai za Wazayuni, ambapo nchi 14 wanachama wa kudumu na wasio wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wametaka kusitishwa mara moja mapigano na kutumwa misaada ya kibinadamu huko Gaza, lakini Marekani imekuwa ikikwamisha juhudi zote za kukomeshwa jinai za Wazayuni kutokana na siasa zake za kuunga mkono bila masharti utawala huo katili.Uungaji mkono wa Jamii ya kimataifa kwa Palestina mara hii ni mkubwa sana na haujawahi kushuhudiwa tena huko nyuma. Kipindi cha miezi 6 ya vita huko Gaza kimekuwa mfano wa kushindwa wazi Jamii ya Kimataifa na wale wanaodai kutetea haki za binadamu katika utekelezaji wa majukumu yao. 

 Siku ya Quds ya mwaka huu inakaribia huku vitendo vya kinyama vya jinai za utawala wa Kizayuni vikidhihirika wazi zaidi kuliko wakati mwingine wowote. Kwa kuzingatia hayo utawala wa Kizayuni unakabiliwa na hali mbaya sana ndani na nje ya utawala huo. Katika upande wa ndani, tofauti za kisiasa zimefikia kilele ambapo mirengo yenye msimamo mikali inaanda mazingira ya kukabiliana wao kwa wao. Kimataifa utawala wa Kizayuni unaendelea kuchukiwa na kutengwa. Utawala wa Tel Aviv umekwama kwenye kinamasi cha Gaza usijue la kufanya. Ndoto ya kuboresha uhusiano na nchi za Kiarabu pia imetoweka kwa kiasi kikubwa. Kwa kuzingatia masuala hayo, tunaweza kusema kwamba Siku ya Quds ya mwaka huu itakuwa ya kipekee katika miongo miwili iliyopita.