Main Title

source : Parstoday
Jumatano

3 Aprili 2024

20:45:44
1448812

Hatua mpya ya BRICS kufuta sarafu ya dola ya Marekani

Jumuiya ya BRICS ya mataifa yanayoibukia kiuchumi inajadili uwezekano wa kubuni mfumo huru wa malipo unaozingatia sarafu za kidijitali ili kupunguza utegemezi kwa mifumo ya fedha ya nchi za magharibi.

Akitangaza mpango huo, mshauri wa rais wa Russia Yury Ushakov alisema kuunda mfumo huru wa malipo wa BRICS ni lengo muhimu kwa siku zijazo, ambalo litategemea utumizi wa sarafu za kidijitali.

Ushakov aliambia shirika la habari la TASS kwamba jambo kuu ni kurahisisha mabadilishano ya kifedha kwa serikali, watu wa kawaida, na biashara.

BRICS ni muungano wa kiuchumi ambao uliundwa mwaka 2009 na tokea mwaka 2010 ulijumuisha Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini. Mwanzoni mwa mwaka huu BRICS ilikubali wanachama wapya ambao ni Misri, Iran, Ethiopia na UAE huku mataifa mengine 44 yakiripotiwa kuonyesha nia ya kujiunga na kambi hiyo.

Mwaka jana, mataifa ya BRICS yaliimarisha biashara ya sarafu za ndani ili kuimarisha uchumi wao na kukabiliana na athari mbaya za ukiritimba wa sarafu ya dola ya Marekani.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mahdi Safari amesema kuunda sarafu ya pamoja katika kundi la BRICS kunaweza kuwa na ufanisi mkubwa.

Nchi za BRICS kwa pamoja zina akiba kubwa ya fedha za kigeni, rasilimali nyingi za asili na idadi ya watu ambayo inachukua zaidi ya 40% ya idadi ya watu ulimwenguni na kwa msingi huo inaweza kuwa  kikundi kikubwa cha kiuchumi na ushawishi mkubwa duniani.

 342/