Main Title

source : Parstoday
Jumatano

3 Aprili 2024

20:46:16
1448813

Mazishi ya washauri wa kijeshi wa Iran waliouawa katika hujuma ya Israel jijini Damascus

Maelfu ya watu wameshiriki katika msafara wa mazishi ya washauri wa kijeshi wa Iran, waliouawa shahidi katika shambulizi la makombora la utawala haramu wa Israel dhidi ya ubalozi mdogo wa Iran katika mji mkuu wa Syria Damascus.

Washiriki wamebeba majeneza ya mashahidi, yakiwa yamepambwa kwa bendera ya taifa la Iran, wakati wa hafla katika Haram takatifu ya Hadhrat Ruqayyah (SA) mjini Damascus Jumanne usiku.

Waombolezaji walisisitiza kuwa watafuata nyazo za mashujaa wa kijeshi wa Iran waliouawa shahidi hadi utakapopromoka mfumo wa ubeberu wa kimataifa na Uzayuni. Sambamba na mazishi hayo, washiriki pia wamehuisha usiku wa Laylatul-Qadr au Usiku wa Hatima. Qur'ani Tukufu iliteremshwa kwa Mtume Muhammad SAW katika usiku kama huo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani takriban karne 14 zilizopita.

Waumini waliokuwa wakiomboleza wameahidi kwamba uchokozi wa Israel hautapita bila kujibiwa.

Aidha waombolezaji hao pia wameapa kwamba damu ya mashahidi haitapotea bure, kwani itawahimiza zaidi Waislamu kupigania kwa nguvu zote ukombozi kamili wa Mji wa al-Quds (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel na baada ya ukombozi huo Waislamu wataswalii swala ya jamaa katika Msikiti wa al-Aqswa.

Waombolezaji aidha wamesisitiza kuwa, adui Mzayuni anafanya jinai zake kutokana na kukata tamaa, kwa sababu amejitumbukiza katika kinamasi huko Ukanda wa Gaza na sasa anatafuta njia ya kujinasua kutoka katika hali hiyo hatari.

Siku ya Jumatatu, ndege za kivita za utawala wa Kizayuni zillishambulia ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus na kuua shahidi washauri wa kijeshi wa Jamhuri ya Kiislamu akiwemo Kamanda wa ngazi za juu wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi  Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) Jenerali Mohammad Reza Zahedi na naibu wake, Mohammad Hadi Haji Rahimi na watu wengine watano.

342/