Main Title

source : Parstoday
Jumatano

3 Aprili 2024

21:00:01
1448821

Mtaalamu wa UN: Israel 'iliwaua kimakusudi' wafanyakazi wa misaada Gaza

Mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya haki za binadamu katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu anasema jeshi la Israel "limewaua kimakusudi" wafanyakazi wa misaada wa Kundi la Misaada la World Central Kitchen, WCK katika Ukanda wa Gaza.

Francesca Albanese alisema hayo katika chapisho la mtandao wa kijamii baada ya wafanyakazi saba wa shirika la misaada la chakula la WCK kuuawa katika shambulio la anga la Israel huko Dayr al-Balah mapema jana Jumanne.

Mtaalamu huyo wa haki za binadamu aliendelea kusema kuwa shambulio la makusudi la jeshi la Israel dhidi ya msafara wa misaada wa WCK, ambao una jukumu la kusambaza msaada wa chakula kati ya watu wa Palestina huko Gaza, lilikuwa na maana ya kuwatia hofu wafadhili wa misaada ya kibinadamu na kuhakikisha njaa inaendelea kuwaua Wapalestina katika eneo la Gaza lililozingirwa.

Albanese katika ujumbe wake ameandika: "Nikijua jinsi Israel inavyofanya kazi, tathmini yangu ni kwamba vikosi vya Israel viliwaua wafanyakazi wa misaada wa WCK kimakusudi ili wafadhili wajitoe na raia wa Gaza waendelee kufa njaa kimya kimya."

Aidha amefafanua sababu ya Israel kuthubutu kuwaua wafanyakazi wa misaada kwa kusema: "Israel inafahamu nchi za Magharibi na baadhi ya nchi za Kiarabu hazitawatetea Wapalestina."

Mtaalamu huyo maalum wa Umoja wa Mataifa amezidi kutoa wito wa vikwazo dhidi ya Israel, huku akibainisha kuwa siku hiyo hiyo ambayo utawala wa Israel uliposhambulia kwa bomu ubalozi wa Iran nchini Syria, uliwaua pia wafanyakazi wa shirika la misaada la WCK.

Ameendelea kusema kuwa: "Israel inavuka kila mstari mwekundu unaowezekana bila kuadhibiwa kikamilifu. Sasa ni wakati wa kuiwekea Israel vikwazo na kuifungulia mashitaka."

Siku ya Jumanne, Ofisi ya Vyombo vya Habari vya Serikali ya Gaza vilisema takriban wafanyakazi saba wa kigeni wa WCK waliuawa katikati mwa Ukanda wa Gaza.

Taarifa hiyo imesema  wafanyakazi wa misaada waliouawa ni pamoja na raia wa Australia, Uingereza, na Poland.