Main Title

source : Parstoday
Jumatano

3 Aprili 2024

21:01:07
1448823

Korea Kaskazini yafanya jaribio la kombora lenye uwezo wa kufika kambi za Marekani bahari ya Pasifiki

Korea Kaskazini imefanya jaribio la kombora la masafa ya kati (IRBM) kutoka pwani yake ya mashariki, kuonyesha dhamira yake ya kuendeleza teknolojia ya makombora yenye uwezo wa kufikia kambi za kijeshi za Marekani katika eneo la Magharibi mwa Bahari ya Pasifiki.

Kombora hilo lililorushwa kutoka eneo karibu na mji mkuu Pyongyang siku ya Jumanne, halikupita Japan kama baadhi ya makombora ya IRBM ambayo Korea Kaskazini iliwahi kurusha, lakini badala yake, lilitua kwenye maji kati ya nchi hizo mbili baada ya kusafiri umbali wa maili 372.

Kanali Lee Sung Joon, msemaji rasmi wa Kamandi ya Majeshi ya Korea Kusini, amesema majaribio kombora hilo yamkini ni mwendelezo wa jaribio la Korea Kaskazini mnamo Machi, ambalo lilihusisha injini ya fueli mango iliyoundwa kwa kombora la hali ya juu la hypersonic la masafa ya kati.

Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida alifahamisha waandishi wa habari kwamba hakujawa na ripoti za uharibifu uliosababishwa na kombora hilo.

Alidai kuwa urushaji wa makombora wa mara kwa mara wa Korea Kaskazini unatishia amani, usalama na utulivu wa Japan, pamoja na usalama wa eneo na wa kimataifa.

Kulingana na wataalamu, ikiwa silaha hizi zitatengenezwa kwa mafanikio, zinaweza kufikia Guam, kituo cha kijeshi cha Marekani cha Pasifiki, na hata mbali zaidi.

Wataalamu wa masuala ya kijeshi wanasema iwapo kutatokea mzozo na Korea Kaskazini, kambi za kijeshi za Marekani nchini Japan na Guam zimewekwa kimkakati kutumika ngome za vikosi vya Marekani. Kulenga vituo hivi ni kipengele muhimu cha mkakati wa vita wa Korea Kaskazini.

 

342/