Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

4 Aprili 2024

14:15:14
1449041

Siku ya Quds na kufichuka sura halisi ya utawala wa mauaji ya kimbari wa Israel

Siku ya Quds mwaka huu 2024 imewadia huku utawala wa Kizayuni wa Israel ukiwa umekwama kwenye kinamasi cha Gaza licha ya mauaji ya kimbari unayoendelea kufanya katika eneo hilo la Palestina.

Ubunifu wa Imam Ruhullah Khomeini (RA) wa kuitambulisha Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kuwa Siku ya Quds Duniani ulikuwa ubifu wa kudumu na wa kihistoria. Baada ya miaka 45 ya ubunifu huo, Siku ya Quds Duniani inaendelea kuadhimishwa kila mwaka kwa adhama na hamasa zaidi kuliko mwaka wa kabla yake duniani kote. Katika siku hii, mwito wa kuitetea na kuiunga mkono Palestina unatolewa na watu wote wanaopigania uhuru duniani, si Waislamu pekee. Suala hili limesababisha hofu na hasira kwa utawala unaoikalia Quds kwa mabavu dhidi ya siku hii ya kimataifa.Siku ya Kimataifa ya Quds 2024 imefika katika hali ambayo mashinikizo dhidi ya utawala wa Kizayuni yamefikia kiwango kisicho na kifani. Ingawa utawala huu unaigiza kama mshindi katika vita vya Gaza, lakini ukweli ni kuwa Israel imeshindwa kabisa katika vita hivyo. Harakati ya Hamas haijatoweka, na uungaji mkono kwa Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa umeongezeka miongoni mwa watu wa Gaza. Wakati huo huo, maandamano ndani ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) yanaendelea, na malalamiko ya familia za mateka wa vita wa Kizayuni wanaoshikiliwa na harakati za mapambano ya ukombozi wa Palestina pia yanaongezeka siku baada ya siku. Vilevile tofauti za kisiasa zimeongezeka ndani ya Israel.

Katika ngazi ya kanda ya Magharibi mwa Asia, hakuna tena athari ya kuanzisha uhusiano kati ya nchi za Kiarabu na utawala wa Kizayuni wa Israel, na mchakato huo sasa umesimama. Safari za kidiplomasia za maafisa wa nchi za Kiarabu kwenda Tel Aviv na kinyume chake, yaani maafisa wa Kizayuni kufanya safari katika baadhi ya nchi za Kiarabu, zimesitishwa.

Katika ngazi ya kimataifa, mashinikizo na chuki ya walimwengu dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel vimeongezeka zaidi kwa sababu ya kudhihirika wazi sura halisi ya kikatili na kinyama ya utawala huo kwa watu duniani. Hata Marekani, ambayo ndiyo muungaji mkono na mfadhili mkuu wa utawala huo ghasibu, imelazimika kujiepusha kupiga kura ya veto dhidi ya azimio la Baraza la Usalama la kusitisha mauaji ya kimbari huko Gaza, hii ikiwa ishara ya hitilafu zilizojitokeza kati ya Tel Aviv na Washington.Kwa kuzingatia hali hiyo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema katika hotuba yake ya siku ya kwanza ya mwaka mpya wa Hijria Shamsia kwamba: “Imebainika waziwazi kuwa utawala wa Kizayuni haukabiliwi tu na mgogoro wa kujilinda, bali pia uko katika mgogoro wa kujiondoa katika mgogoro huo; Umekwama kwenye kinamasi, hauwezi kujiokoa. Kuingia utawala wa Kizayuni huko Gaza kuliutumbukiza utawala huo kwenye kinamasi; Hii leo ukiondoka Gaza atakuwa umeshindwa, na ukibakia huko pia atashindwa. Hii ndiyo hali halisi ya utawala wa Kizayuni." Hapana shaka kuwa, Ijumaa ya kesho, ambayo ni ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, itakuwa moja ya siku ngumu zaidi kwa Wazayuni, kwa sababu bango kubwa la hasira na chuki ya walimwengu dhidi ya utawala huo haramu itaonekana zaidi kuliko wakati mwingine wowote katika kona zote za dunia.

342/