Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

4 Aprili 2024

14:21:07
1449049

Baraza la Haki za Kibinadamu la UN lapanga vikwazo vya silaha dhidi ya Israel

Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa (UNHRC) litachunguza rasimu ya azimio la kuweka vikwazo vya silaha dhidi ya utawala haramu wa Israel.

Rasimu hiyo imewasilishwa na Pakistan kwa niaba ya nchi 55 kati ya 56 wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC). Itajadiliwa Ijumaa wiki hii kwa misingi kwamba kuna "hatari ya mauaji ya kimbari huko Gaza."

Rasimu hiyo ya kurasa nane inafadhiliwa na Bolivia, Cuba na ujumbe wa Palestina huko Geneva. Inalaani hatua ya Israel kutumia silaha za milipuko zenye athari katika maeneo yenye watu wengi ya Ukanda wa Gaza. Pia inataka Israel “itekeleze wajibu wake wa kisheria wa kuzuia mauaji ya halaiki.”

Kupitishwa kwa rasimu ya azimio hilo kutafanya iwe mara ya kwanza kwa chombo cha juu cha haki cha Umoja wa Mataifa kuchukua msimamo kama huo kuhusu Gaza tangu mapema Oktoba mwaka jana.

Rasimu hiyo inaitaka Israel kukomesha kukalia kwa mabavu ardhi ya Palestina, na kuondoa mara moja "vizuizi haramu" na aina nyingine zote za "adhabu ya pamoja."

Israel imewaua zaidi ya Wapalestina 32,900, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na kuwajeruhi wengine karibu 75,500 huko Gaza tangu Oktoba 7. Pia imekata mafuta, umeme, chakula na maji kwa Wapalestina wanaoishi eneo hilo.

Kwa mujibu wa shirika la Euro-Med Human Rights Monitor, jeshi la Israel hadi sasa limeua zaidi ya watoto 14,400 huko Gaza, ikiwa na maana kwamba, watoto ni zaidi ya theluthi moja ya watu waliouawa na Israel katika eneo hilo.

Israel pia inawaua watu kwa njaa kwa makusudi huko Gaza kwa kuharibu chakula na kuzuia misaada ya chakula, dawa na bidhaa zingine za binadamu.

Kulingana na Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya Stockholm (Sipri), Marekani bado inasalia kuwa mfadhili mkuu wa Israel, ikichangia karibu asilimia 70 ya uagizaji wa silaha zake kati ya 2013 na 2022.

342/