Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

5 Aprili 2024

14:46:18
1449242

Kiongozi wa Ansarullah: Tumeshambulia meli 90 zinazohusiana na Israel katika Bahari ya Sham

Katibu Mkuu wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen Sayyid Abdul Malik Badruddin al-Houthi amesema, wapiganaji wa harakati hiyo wameshambulia meli 90 za Israel au zile zinazoelekea bandari za utawala huo wa Kizayuni katika eneo la Bahari ya Sham mbali na kuongeza na kupanua wigo wa mashambulio ya ndege zisizo na rubani katika maeneo mengine.

Katika hotuba aliyotoa usiku wa kuamkia leo, Abdul Malik al Houthi ameeleza kwamba wanamuqawama wa Ansarullah wamefanya mashambulizi 34 kwa mwezi mmoja, wakitumia makombora 125 ya balestiki na ndege zisizo na rubani. Harakati hiyo ya Wahouthi, ambayo inadhibiti mji mkuu wa Yemen, Sana'aa na maeneo yenye wakazi wengi zaidi, imeshambulia meli za kimataifa katika Bahari ya Sham tangu mwezi Novemba kuonyesha mshikamano na Wapalestina waliozingirwa wa Ukanda wa Ghaza, na kupelekea kuandamwa na hujuma na mashambulio ya Marekani na Uingereza, waungaji mkono wakuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Kuhusiana na hilo, Kiongozi wa Ansarullah ya Yemen amebainisha katika hotuba yake kwamba, watu wapatao 37 wameuawa na wengine 30 wamejeruhiwa katika mashambulizi 424 ya anga, yaliyofanywa na Marekani na Uingereza ndani ya ardhi ya Yemen katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita tokea Februari.

 Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Abdul Malik al Houthi amesema, hatua ya Marekani ya kuendelea kuupatia silaha utawala wa Kizayuni unaofanya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Ghaza imefichua na kuweka wazi unafiki wa Washington.

Aidha amesisitiza kuwa, Yemen itaendeleza operesheni zake za kuiunga mkono Palestina, ambazo zimeshuhudia wanajeshi wa Yemen wakishambulia meli za Israel au zenye mfungamano na utawala huo haramu.

Sayyid Abdul Malik al Houthi amesema: "kambi yetu ya Yemen inaendeleza operesheni zake za kijeshi katika Bahari ya Sham, Bahari ya Arabia na hata kufikia Bahari ya Hindi".../ 

342/