Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

5 Aprili 2024

14:51:49
1449247

Khatibu wa Sala ya Ijumaa mjini Tehran: Utawala wa Kizayuni ni nembo ya jinai

Khatibu wa muda wa Sala ya Ijumaa Tehran ameashiria jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel katika mauaji ya wanawake na watoto wa Kipalestina na kusema: "Utawala bandia wa Kizayuni unaoua watoto sasa umebadilika na kuwa nembo ya jinai katika mfumo wa kisheria wa kimataifa.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IRIB, Hujjatul Islam Sayyed Mohammad Hasan Abu Turabifard, khatibu wa muda wa Swala ya Ijumaa mjini Tehran leo, katika khutba zake za sala ya Ijumaa, ameyataja matembezi ya Siku ya Kimataifa ya Quds kama uungaji mkono mkubwa na usio na kifani  kwa wtu shupavu wa Palestina na Mujahidina walio mstari wa mbele wa vita katika ukanda wa Gaza na kuongeza kuwa: "Mauaji ya kimbari ya Wapalestina wasiojiweza na uharibifu wa makazi zaidi ya 70,000, mamia ya misikiti na shule na vyuo vikuu na uharibifu wa hospitali 22, kuzingirwa kabisa kwa Ukanda wa Gaza, ni jinai ambazo zimeufanya utawala bandia wa Israel, ambao ni muuaji ya watoto, kuwa nembo ya jinai katika Mfumo wa sheria za kimataifa."

Khatibu wa Sala ya Ijumaa Tehran ameeleza kuwa operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa  iliyoanzishwa na wanamuqawama na wapigania ukombozi wa Palestina mnamo Oktoba 7, 2023 iliibua zilzala katika muundo wa kijeshi, kisiasa na kiuchumi wa utawala wa Kizayuni wa Israel na waungaji mkono wake. Ameongeza kuwa hivi sasa hadhi ya kimataifa na ya kieneo ya Marekani inakabiliwa na tishio huku utawala wa Kizayuni wa Israel ukikaribia kushindwa.

Hujjatul Islam Abu Turabi Fard, amekosoa mwelekeo wa nchi za magharibi kuhusu haki za binadamu na kusema: "Wapalestina wameonyesha maadili ya juu ya Uislamu katika uwanja wa vita ambavyo havina mlingano. Muqawama au mapambano ya kipekee ya Wapalestina yanastahiki kupongezwa katika hali ambayo utawala wa Israel baada ya miezi sita ya vita dhidi ya Gaza haujapata chochote isipokuwa kutekeleza mauaji ya kimbari."Akiashiria kitendo cha kigaidi cha utawala wa Kizayuni katika shambulio dhidi ya ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus, khatibu wa muda wa Sala ya Ijumaa ya mjini Tehran amekitaja kitendo hicho kuwa ni jaribio la Israel la kutaka kujinasua kutoka katika kinamasi cha vita vya Gaza.

 Hujjatul Islam Abu Turabi Fard ameongeza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itajibu kikamilifu, kwa busara, kwa nguvu imara na kwa kiwango sawa na kile cha mashambulizi ya adui. Khatibu wa Swala ya Ijumaa ya mjini Tehran ameeleza kuwa, Iran imekuwa na nguvu kubwa ya kitaifa na kieneo na imeweza kuifanya kadhia ya Palestina iwe muhimu zaidi ulimwengu wa Kiislamu. Aidha amesema Utawala wa Kizayuni unakabiliwa wapiganaji shupavu na wenye umoja wa harakati za kupigania ukombozi wa Palestina za Hamas na Jihad Islami ambazo zina itikadi na stratijia moja na iliyoratibiwa ya kijeshi.

342/