Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

5 Aprili 2024

14:53:36
1449249

Mtazamo wa wachambuzi wa mambo kuhusu mashambulio ya kigaidi kusini mashariki mwa Iran

Mkoa wa Sistan na Baluchistan wa kusini mashariki mwa Iran, kwa mara nyingine tena umekumbwa na mashambulizi ya kigaidi yaliyofanywa na genge linaloungwa mkono na utawala wa Kizayuni wa Israel na Marekani.

Wakati tunaandaa uchambuzi huu wa kisiasa, hali ya usalama ilikuwa imesharejea kama kawaida, magaidi 15 walikuwa wameshaangamizwa, na operesheni ya kusafisha mabaki ya magaidi hao ilikuwa inaendelea. 

Hayo yalitangazwa na Kamanda wa Kikosi cha Nchi Kavu cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH), Brigedia Jenerali Mohammad Pakpour ambaye alisema kuwa, hadi wakati anatoa taarifa hiyo, magaidi 15 walikuwa wameshaangamizwa katika operesheni za kuzima mashambulizi matatu ya kigaidi yaliyofanywa na magaidi hao kusini mashariki mwa Iran.

Genge la kigaidi la "Jaish al Dhulm" linaloungwa mkono na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel, usiku wa kuamkia jana Alkhamisi lilifanya mashambulizi ya kigaidi kwa wakati mmoja katika vituo mbalimbali vya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran SEPAH katika miji ya Rask na Chabahar, kusini mashariki mwa Iran, lakini mashambulizi yote hayo yalizimwa na vikosi vya kulinda usalama wa taifa vya Iran mwanzoni kabisa kwa kuanza kwake. 

Shirika la habari la Iran Press lilimnukuu Brigedia Jenerali Mohammad Pakpour akisema jana Alkhamisi kwamba, magaidi walioshiriki kwenye uvamizi huo wote walikuwa wamevaa vizibao vya kujiripua kwa mabomu na kuna uwezekano idadi ya magaidi walioangamizwa ikaongezeka. 

Wachambuzi mbalimbali wa masuala kama hayo wametoa maoni kuhusu shambulio hilo la kigaidi akiwemo Ismail Baqheri ambaye amesema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni imara sana katika masuala ya ulinzi na kukabiliana na vitendo vya kigaidi kutokana na kuwa ni muhanga mkuu wa mashambulizi ya kigaidi. Ni kwa sababu hiyo ndio maana mashambulizi kadhaa ya Jumatano usiku ya magaidi wanaoungwa mkono na Marekani na Israel yalizimwa mara moja katika mkoa wa Sistan na Baluchistan wa kusini mashariki mwa Iran. Kwa upande wake, Alireza Marhamati, Naibu Gavana wa mkoa wa Sistan na Balichustan anayesimamia masuala ya usalama na utekelezaji sheria mkoani humo amesema kuwa, mashambulio ya kigaidi kwenye makao makuu mawili ya kijeshi katika miji ya Rask na Chabahar mkoni humo yamezimwa mwanzoni kabisa mwa kuanza kwake na hali katika maeneo hayo yamedhibitiwa na vikosi vya kulinda usalama vya Iran.

 Wachambuzi wengine wanasema kuwa, lengo la genge hilo la kigaidi na mabwana zao wa Magharibi na utawala wa Kizayuni ni kutaka kuonesha kuwa mkoa huo wa kusini mashariki mwa Iran unaopakana na Pakistan, hauko salama, na vile vile kujaribu genge hilo kujionesha lina nguvu za kufanya mashambulizi ndani ya Iran. Lengo jingine la magaidi hao na mabwana zao ni kuwakosesha utulivu na amani wananchi Waislamu wa Iran wakiwemo wa maeneo hayo ya kusini mashariki mwa nchi hasa wakati huu wa mwezi mtukufu wa Ramadhani tena katika kipindi hiki cha mikesha ya Laylatul Qadr, lakini njama za maadui hao wa Iran ya Kiislamu zimeshindwa na haziwezi kuvunja moyo na imani ya wananchi wakiwemo wa mkoa wa Sistan na Baluchistan; na muda wote wananchi hao wamesimama imara kukabiliana na njama hizo za maadui. Tunapenda kukumbusha hapa kwamba, baada ya kutiwa mbaroni na kuangamizwa aliyekuwa kiongozi wa genge la kigaidi la Jaish al Shaitan, Abdul Malik Rigi, kaka yake Abdul Hamid na baadhi ya viongozi wa genge hilo nchini Iran na Pakistan, mabaki ya magaidi wa genge hilo yanaendelea kufanya jinai chini ya jina la Jaish al-Dhulm lenye uhusiano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda katika pembe tofauti za mkoa wa Sistan na Baluchistan na mara zote yanatokea katika ardhi ya Pakistan na kujipenyeza kwenye ardhi ya Iran na baadaye kukimbilia kwenye ardhi ya Pakistan kujificha na kupanga njama nyingine dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Lakini kama wanavyosema wachambuzi wa mambo, njama hizo haziwezi kuteteresha imani thabiti ya wananchi wa Iran.

342/