Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

5 Aprili 2024

14:55:49
1449253

Wanasheria zaidi ya 600 waionya Uingereza: Kuipatia silaha Israel ni ukiukaji wa sheria za kimataifa

Zaidi ya wanasheria 600 wa Uingereza, wakiwemo majaji watatu wa zamani wa Mahakama ya Juu, mawakili, wasomi, na majaji wakuu wastaafu, wameonya kwamba hatua ya serikali ya Uingereza ya kuupatia silaha utawala wa Kizayuni wa Israel inakiuka sheria za kimataifa.

Kwa mujibu wa gazeti la Irish Times, wanasheria hao wameeleza katika barua ya wazi waliyomwandikia waziri mkuu wa Uingereza Rishi Sunak: "wakati tunakaribisha wito unaozidi kuwa na uzito unaotolewa na serikali yako wa kusitishwa mapigano na kuingizwa misaada ya kibinadamu Ghaza bila kizuizi; wakati huo huo, kuendeleza uuzaji wa silaha na mifumo ya silaha kwa Israel na kukazania kutoa vitisho vya kusimamisha msaada wa Uingereza kwa UNRWA kunazidi kuifanya serikali yako ikwepe kutekeleza sheria za kimataifa”.  Barua hiyo imeashiria indhari ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kwamba kuna hatari kubwa ya uwezekano wa Israel kufanya mauaji ya kimbari huko Ghaza na kueleza kwamba: "ni lazima Uingereza ichukue hatua za haraka kukomesha kwa njia za kisheria vitendo vinavyosababisha hatari kubwa ya kufanywa mauaji ya kimbari".Sehemu nyingine ya barua hiyo imesema, kushindwa Uingereza kutekeleza majukumu yake kulingana na mkataba wa mauaji ya kimbari kwa kutochukua hatua zote zilizo ndani ya uwezo wake za kuzuia mauaji ya halaiki kutaibebesha serikali hiyo dhima ya kufanya makosa ya kimataifa, ambayo yatalazimu kulipiwa fidia kamili.

 Kwa mujibu wa Irish Times, barua hiyo imetiwa saini na majaji wakuu wastaafu ambao kwa kawaida hujiepusha kutoa maoni yao hadharani kuhusu masuala nyeti ya kisiasa. Waliotia saini barua hiyo ni pamoja na majaji wa zamani wa Mahakama ya Juu Lord Sumption na Lord Wilson, Majaji wa zamani wa Mahakama ya Rufaa Sir Stephen Sedley, Sir Alan Moses, Sir Anthony Hooper, na Sir Richard Aiken, na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili wa Uingereza na Wales Matthias Kelly KC.../

342/