Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

5 Aprili 2024

14:57:17
1449255

Siku ya Quds; ubunifu wa kimataifa na mojawapo ya mifano ya kihistoria ya uungaji mkono wa Iran kwa Palestina

Siku ya Kimataifa ya Quds ni ubunifu wa kwanza ulioonyeshwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika uga wa siasa za nje mara tu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Moja ya hatua muhimu na za kistratijia zinazochukuliwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kuunga mkono mapambano ya ukombozi wa Palestina ni kutoutambua rasmi utawala wa Kizayuni.

Uhusiano kati ya Tehran na Tel Aviv ambao ulikuwa ukiendelea kimfumo na kwa njia rasmi kabisa kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, ulipitia mabadiliko ya kimsingi baada ya ushindi wa mapinduzi hayo. Miaka 45 baada ya ushindi wa Mapinduzi, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran si tu haijautambua rasmi utawala wa Kizayuni, bali inasisitiza udharura wa kuangamizwa utawala huo bandia. Stratejia hiyo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imechangia pakubwa katika kuhuisha suala la Palestina katika ulimwengu wa Kiislamu, kuibua na kuimarisha mhimili wa mapambano katika eneo la Asia Magharibi na pia kupelekea mataifa ya Kiislamu kuchukizwa na utawala wa Kizayuni.

Aidha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haijawahi kuwa na mbinu fiche katika kuiunga mkono Palestina na daima imekuwa ikitoa uungaji mkono wa wazi kwa harakati za ukombozi wa Palestina na Quds Tukufu. Hatua ya Imam Khomeini ya kuitaja Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kuwa Siku ya Kimataifa ya Quds ni moja ya mifano ya uungaji mkono wazi wa Iran kwa Palestina.

Ubunifu huo mbali na kuwa ni uungaji mkono wa wazi kwa Palestina, lakini pia ni mwiba na machungu ya kudumu kwa utawala wa Kizayuni, kwa sababu kila mwaka katika siku hii, mataifa ya Kiislamu na hata yasiyo ya Kiislamu hufanya maandamano makubwa kote duniani kwa ajili ya kuunga mkono na kuitetea Palestina. Uungaji mkono huo kwa Palestina umeendelea kwa nguvu kubwa zaidi katika kipindi hiki cha uongozi wa Ayatullah Khamenei, ambaye pia ametangaza kwa sauti kubwa uungaji mkono wake kwa taifa hilo linalodhulumiwa. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu tarehe 24 Novemba 2018 alisisitiza katika kikao na viongozi wa ngazi za juu wa Mfumo wa Kiislamu, wageni wa Kongamano la Wiki ya Umoja wa Kiislamu na mabalozi wa nchi za Kiislamu kuwa: “Msimamo wetu kuhusu suala la Palestina ni msimamo wa kimsingi na thabiti. Kabla ya ushindi wa Mapinduzi, mwanzoni mwa harakati za Mapinduzi, Imam alifafanua hatari ya ushawishi, uingiliaji na ukandamizaji wa Uzayuni. Jambo la kwanza ambalo Jamhuri ya Kiislamu ililifanya mara tu baada ya ushindi wa Mapinduzi ni kuchukua kituo cha Wazayuni mjini Tehran na kukikabidhi kwa Wapalestina, na bado tunashikilia msimamo huo huo. Tunaiunga mkono Palestina, tunawasaidia Wapalestina na tutaendelea kuwasaidia, na wala hatufanyi mzaha kuhusu suala hili. Ulimwengu wote wa Kiislamu unapaswa kuisaidia Palestina."

 Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia inawaunga mkono kwa dhati Wapalestina katika asasi za kieneo kama vile Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu na jumuiya za kimataifa kama vile Umoja wa Mataifa na kuzishawishi nchi nyingine zifuate mfano huo. Wakati huo huo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran miaka yote imekuwa mwenyeji wa mikutano na makongamano mengi ya kuunga mkono Palestina, jambo ambalo limewavutia wasomi wa nchi nyingi za dunia hususan za Kiislamu. Uungaji mkono huo madhubuti wa Iran kwa wananchi madhulumu wa Palestina na kadhia ya Palestina ndiyo sababu kuu ya hasira ya utawala wa Kizayuni na nchi za Magharibi, hususan Marekani dhidi ya serikali ya Tehran.


342/