Main Title

source : Parstoday
Jumapili

7 Aprili 2024

14:39:15
1449777

Kiwewe cha Wazayuni wakisubiri jibu la kijeshi la Iran kutokana na jinai zao

Utawala wa Kizayuni umesema una wasiwasi na jibu liltakalotolewa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kufuatia jinai za karibuni iliyofanywa na utawala huo ya kuishambulia sehemu ya jengo la ubalozi dogo wa Iran huko Syria. Kwa kuhofia jibu la kijeshi la Iran, utawala wa Kizayuni umetoa amri ya kufungwa balozi zake katika maeneo mbalimbali duniani.

Shirika la Redio na Televisheni la Israel limetangaza kuwa, utawala huo umeamua kuzihamisha kwa muda balozi zake zote duniani kutokana na hofu ya uwezekano wa Iran kujibu mashambulizi ya hivi karibuni ya kigaidi ya Tel Aviv katika eneo moja la  ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus, Syria. Baadhi ya duru za Kizayuni juzi usiku ziliripoti kuwa balozi saba za Israel duniani ukiwemo wa Bahrain, Misri, Jordan, Morocco na Uturuki zimefungwa kwa kuhofia shambulio la kulipiza kisasi la Iran. Wakati huo huo Wazayuni wenyewe wamekiri kuwa wanajeshi wa utawala huo wamewekwa katika hali ya tahadhari kikamilifu baada ya Israel kushambulia ubalozi mdogo wa Iran huko Syria. Televisheni inayorusha matangazo kwa lugha ya Kiibrania ya Kan pia imeripoti kuwa wanajeshi wa utawala wa Israel wamejiweka tayari katika mipaka ya kaskazini mwa Lebanon na kuchukua tahadhari kubwa huko Tel Aviv na katika miji mingine huku utawala huo ukifuta likizo kwa wanajeshi wake kwa kuzingatia kuwepo uwezekano wa Iran kufanya shambulizi la kulipiza kisasi. Jumatatu usiku, saa moja baada ya shambulio la Israel dhidi ya ubalozi mdogo wa Iran nchini Syria, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitangaza kuwa utawala wa Israel umekiuka wazi  Mkataba wa Umoja wa Mataifa, sheria za kimataifa na mamlaka ya kujitawala ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Syria na ina haki ya kujibu  uhalifu huo. Wawakilishi wa nchi wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pia siku ya Jumanne waliitisha kikao cha dharura na kulaani shambulio la Israel katika jengo la ubalozi mdogo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huko Damascus, Syria. Walisema kuwa, kitendo hicho cha Israel ni ukiukaji mkubwa wa Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961, ambao unasisitiza kulindwa na kuheshimiwa vituo vya kidiplomasia, na wakatahadharisha kuhusu matokeo mabaya ya jinai zilizo kinyume na sheria za utawala huo katika eneo hili. Siku tatu zilizopita pia maafisa wa ngazi ya juu wa kisiasa na kijeshi wa Iran walitoa matamko kwa nyakati mbalimbali na kusisitiza  kuwa Tehran itajibu haraka na kwa nguvu jinai hiyo ya Wazayuni.  Jumatatu alasiri iliyopita ndege za kivita za utawala wa Kizayuni ziliushambulia kwa mabomu ubalozi mdogo wa Iran huko Damascus Syria, ambapo washauri saba wa kijeshi wa Iran waliokuwa wakihudumu nchini Syria waliuliwa shahidi katika jinai hiyo ya Israel. Utawala wa Kizayuni umefanya jinai hiyo dhidi ya ubalozi mdogo wa Iran kufuatia kushindwa mtawalia kukabiliana na muqawama wa Palestina na kusimama ngangari raia wa Kipalestina wa Ukanda wa Gaza. Jengo la ubalozi mdogo wa Iran huko Damascus limebomoka kikamilifu huku sehemu nyingine za jengo la ubalozi pia zikidhurika na kupata hasara. Maeneo mbalimbali ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na Israel yamekumbwa na hofu na wahka kufuatia shambulio lililofanywa na Israel katika kituo cha kidiplomasia cha Iran huko Syria, na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kusisitiza kuwa ina haki ya kujibu jinai hiyo. 

Alum David, mwandishi wa habari wa Israel ameandika katika  mtandao wa kijamii kwamba duru za usalama na kijeshi za Israel zinasubiri Iran kuishambulia Israel. Katika kujibu hatua ya Israel ya kushambulia sehemu ya ubalozi mdogo wa Iran nchini Syria, Sima Shain, mmoja wa maafisa wa zamani wa shirika la kijasusi la Israel la Mossad amesema kuwa Iran ina uwezo wa kutosha wa kujibu na kutoa kipigo kikali kwa Israel kwa kubuni  operesheni kubwa;  na kwamba  maafisa Waisraeli hawapasi kudharau uwezo wa Iran. Ingawa tangu tarehe 7 Oktoba utawala wa Kizayuni ulipoanzisha duru mpya ya mashambulizi  katika ardhi za Palestina hususan Gaza, utawala huo umekuwa ukilenga maeneo ya Syria na Lebanon mbali na ardhi za Palestina kwa kisingizio cha kulenga upande wa muqawama, lakini shambulio la hivi karibuni la utawala huo katika kituo cha kidiplomasia cha Iran huko Syria ni nukta kuu katika jinai za utawala huo ghasibu, na  dharau ya wazi kwa msingi wa sheria zilizokubaliwa na jamii ya kimataifa yaani, kinga ya mabalozi na kulindwa  maeneo ya kidiplomasia na ubalozi. Jinai hii ambayo Israel imeifanya huku utawala huo ukikabiliwa na mashinikizo ya  kimataifa ili uitishe vita dhidi ya Gaza inaonesha kiburi cha utawala huo haramu na namna  unavypuuza  wito wa kimataifa wa kusitisha vita dhidi ya Gaza.Ingawa baadhi ya weledi wa mambo wanatathmini madhumuni ya ya kutkelezwa jinai hii tajwa na Israel kama jaribio la kuliingiza eneo lote a Mashariki ya Kati kwenye mgogoro, lakini wahusika na waungaji mkono wa jinai hii tajwa wanapaswa kutambua kwamba hatimaye watalazimika kulipa gharama kubwa kwa jinao zao hizo; na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia imetangaza kuwa ina haki ya kujibu kwa wakati na mahali muafaka jinai hiyo mpya ya Wazayuni. 

342/