Main Title

source : Parstoday
Jumapili

7 Aprili 2024

14:41:35
1449781

Kuongezeka mashinikizo dhidi ya serikali ya Biden kwa ajili ya kupungaza uungaji mkono wake kwa utawala wa Kizayuni

Kuendelea vita vya Ghaza na jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wasiokuwa na hatia wa eneo hilo na hasa mauaji ya kimbari na utumiaji njaa kama silaha, kumezidisha mashinikizo ya ndani kwa serikali ya Biden ya kumtaka apunguze uungaji mkono wake kwa Tel Aviv, na wakati huo huo, kuongeza pia tofauti kati ya Ikulu ya White House na Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni.

Kuhusiana na jambo hilo, wabunge 40 wa chama cha Democratic katika Congress ya Marekani wamemtaka Rais Joe Biden wa nchi hiyo asitishe uuzaji wa silaha kwa utawala wa Kizayuni, ambapo jina la Nancy Pelosi, spika wa zamani wa bunge hilo linaonekana kati ya wabunge hao. Barua waliyomwandikia Rais Biden inamtaka asimamishe uuzaji wa silaha kwa utawala wa Kizayuni na kuweka masharti kwa ajili ya kutolewa misaada ya Washington kwa utawala huo.

Kusainiwa barua hiyo na wawakilishi hao wa Congress ya Marekani, haswa Pelosi, ambaye ni mmoja wa maafisa muhimu wa chama cha Democratic katika historia ya nchi hiyo na ambaye amekuwa mtetezi mkuu wa uhusiano wa Marekani na Israeli kwa miongo kadhaa, kunaonyesha ni kwa kiwango gani jinai za utawala wa Kizayuni na vitendo vyake vya kinyama huko Ukanda wa Ghaza vimeathiri fikra za wananchi wa Marekani nchini. Wakati huo huo, takwa la wabunge 40 wa chama cha Democratic kwa Biden la kusimamisha uuzaji silaha kwa Israel linaonyesha haja ya kutazamwa upya sera za jadi za wabunge wa Marekani kuhusiana na utawala wa Kizayuni, ambazo zinaegemea zaidi katika uungaji mkono wa pande zote kwa Tel Aviv katika vita vya Ghaza.Baadhi ya maseneta wa Marekani wamechukua pia msimamo kama huo. Bernie Sanders, Seneta wa kujitegemea wa Marekani hivi karibuni alimtahadharisha Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa Israel, na kusema kwamba iwapo itaendelea kushambulia misafara ya misaada ya kibinadamu inayoingia Ukanda wa Ghaza, Marekani itasimamisha misaada yake yote ya kijeshi kwa utawala huo. Vilevile, Tim Kane, Seneta wa chama cha Democratic wa Marekani amesisitiza kuwa, kutumwa silaha katika ardhi zinazokaliwa kwa mbavu  kutazidisha tu mateso na machungu ya wananchi wa Ghaza na kuvurunga zaidi hali ya mambo katika eneo hilo na hivyo kuitaka Marekani isimamishe mpango wake wa kutuma silaha kwa utawala huo. 

Katika upande mwingine, hitilafu kati ya Ikulu ya Marekani na Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni, kuhusiana na mchakato wa vita vya Ghaza, zimesababisha kutokea mvutano wa wazi kati ya Biden na Netanyahu. Katika muktadha huo, NBC iliripoti, ikiwanukuu maafisa wa Marekani, kwamba Biden alimsisitizia  Netanyahu kwamba ikiwa hatakubali kusitisha mapigano katika Ukanda wa Ghaza, uhusiano wa pande hizo utachukua mkondo tofauti kabisa. Jarida la Axios pia liliripoti, likinukuu vyanzo vya habari, kwamba mawasiliano ya simu ya hivi karibuni kati ya Biden na Netanyahu yalikuwa magumu zaidi tangu Oktoba 7 2023. Pamoha na hayo lakini Biden hakuashiria katika mazungumzo hayo ya simu na Netanyahu, suala la uwezekano wa kukatwa misaada ya Washington kwa Tel Aviv. Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, Biden alimuonya Netanyahu kwamba serikali ya Marekani haitaendelea kumuunga mkono hadi pale Israel itakapotazama upya sera zake huko Ghaza. Gazeti la lugha ya Kiibrania la Israel Aliyum pia lilitangaza kuwa katika mazungumzo na Netanyahu, Biden kwa mara ya kwanza tangu kuanza vita huko Ghaza, alitoa wito wa kusitishwa mara moja mapigano ili kuboresha hali ya kibinadamu katika ukanda huo. Gazeti hilo lilitaja takwa hilo kuwa pigo kubwa kwa Israeli.Bila shaka vitisho hivyo vya kidhahiri tu vya serikali ya Biden kama kawaida vimepuuzwa na utawala wa Kizayuni na baraza la mawaziri la vita la utawala huo, ambapo watawala wa Kizayuni akiwemo Benjamin Netanyahu, bado wanasisitiza juu ya ulazima wa kuishambulia vikali Rafah kusini mwa Gaza kwa kisingizio cha kuyaangamiza makundi ya muqawama ya Palestina, jambo ambalo bila shaka litazidhisha maafa ya kibinadamu dhidi ya Wapalestina wasio na hatia. Marekani inahesabiwa kuwa muungaji mkono mkubwa zaidi wa utawala wa Kizayuni na jinai zake katika Ukanda wa Ghaza, katika nyanja zote za kisiasa na kimataifa na pia katika kuupa silaha za maangamizi. Hata hivyo, kutokana na kuongezeka mashinikizo ya fikra za waliowengi duniani na ndani ya Marekani yenyewe kuhusu kuendelea jinai za utawala huo katika vita vya Ghaza, utawala wa Biden sasa unajifanya kujali maslahi ya kibinadamu ili kuboresha sura yake na kumdhaminia kura za Wamarekani katika uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika baadaye mwaka huu.

342/