Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

8 Aprili 2024

20:11:25
1450076

WHO: Hali ya hospitali ya al-Shifa katika mji wa Gaza ni ya kutisha

Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema kuwa hali ya hospitali ya al Shifa katika mji wa Gaza ni ya kutisha na mbaya sana.

Shirika la WHO limeripoti kuwa hospitali ya al Shifa huko magharibi mwa Ukanda wa Gaza imegeuka kuwa jengo lililojaa miili ya mashahidi iliyoharibika, katika hali ambayo hospitali hiyo iliwahi kutoa huduma nyingi zaidi za matibabu katika Ukanda Gaza.  

Timu ya misaada na matibabu ya Shirika la Afya Duniani hatimaye Ijumaa iliyopita iliweza kuingia katika hospitali ya al Shifa baada ya kushindwa kwa mara kadhaa kuingia hospitalini hapo tangu Machi 25. 

Ripoti ya WHO imeeleza kuwa,  hakuna mgonjwa aliyesalia hospitalini na makaburi ya kina yalichimbwa nje ya kitengo cha huduma za dharura cha hospitali hiyo na katika majengo ya upasuaji. Aidha miili mingi imezikwa kwa upande mmoja huku miili ya wahanga ikionekana wazi.  

Shirika la Afya Duniani limeendelea kueleza kuwa, ni muhimu kulinda heshima ya mtu hata wakati wa kifo, na kwamba kiasi cha uharibifu na maafa yaliyosabababishwa na utawala ghasibu wa Israel umepelekea kituo hicho cha matibabu kushindwa kutoa huduma kikamilifu.  

Dakta Tedros Adhanom  Gebreyesus Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X kwamba: Wawakilishi wa WHO na washirika wao wamefanikiwa kuingia katika hospitali ya al Shifa ambayo hapo awali ilikuwa uti wa mgongo wa mfumo wa afya wa Gaza, na sasa imekuwa jengo tupu na kaburi la binadamu baada ya kuzingirwa hivi karibuni. Hii ni katika hali ambayo ripoti ya WHO inaeleza kuwa sasa ni hospitali 10 tu huko Gaza ambazo zinatoa huduma kwa kiwango fulani kati ya hospitali kuu 36 za eneo hilo. 

342/