Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

8 Aprili 2024

20:12:14
1450078

Vikosi vya Yemen vyashambulia meli za Uingereza, Israel, meli za kijeshi za Marekani katika Bahari ya Sham

Msemaji wa Jeshi la Yemen amesema vikosi vya wanamaji vya nchi hiyo vimefanya operesheni nyingi dhidi ya meli za kibiashara za Uingereza na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Vikosi vya Yemen pia vimelenga manowari za Jeshi la Marekani katika pwani ya taifa hilo la Kiarabu ili kuwaunga mkono Wapalestina wakati huu Israel inapendeleza  vita vya mauaji ya dhidi ya Wapalestina wa Gaza kwa himaya ya Marekani na Uingereza.

Akizungumza katika kikao cha wanahabari kilichorushwa hewani moja kwa moja kutoka mji mkuu wa Yemen, Sana'a siku ya Jumapili, Brigedia Jenerali Yahya Saree amesema vikosi vya nchi hiyo vimeishambulia meli ya mizigo ya Uingereza ya HOPE ISLAND katika Bahari ya Sham..

Amebainisha kuwa meli hiyo ilipigwa kwa makombora maalumu ya jeshi la wanamaji, akisisitiza kuwa meli hiyo ililengwa kwa kombora moja kwa moja.

Vikosi vya wanamaji vya Yemen pia vimelenga meli ya mizigo ya Israel, MSC GRACE F katika Bahari ya Hindi. Yahya Saree pia amedokeza kuwa wamelenga meli nyingine ya mizigo ya Israel, MSC GINA katika Bahari ya Arabia.

Afisa huyo wa ngazi ya juu wa kijeshi nchini Yemen amebainisha kuwa operesheni hizo zilifanywa kwa makombora kadhaa ya balistiki na mengineyo, akisisitiza kwamba shabaha zilizolengwa zilipigwa kwa usahihi.Zaidi ya hayo, vikosi vya wanamaji vya Yemen vimetumia ndege kadhaa zisizo na rubani wakati wa operesheni mbili tofauti katika Bahari ya Sham, zikilenga meli kadhaa za kijeshi za Marekani.

Saree amesisitiza kwamba mashambulizi hayo ya makombora yamefanyika kwa ajili ya kuwaunga mkono Wapalestina wanaodhulumiwa huko Gaza na kujibu hujuma za pamoja za Marekani na Uingereza dhidi ya Yemen.

Amesema wanajeshi wa Yemen wataendelea na operesheni zao za kijeshi, na watazuia meli zinazomilikiwa na Israel au zile zinazoelekea katika  bandarini zinazokaliwa kwa mabavu na Israel hadi pale usitishaji vita wa kudumu utakapotekelezwa katika Ukanda wa Gaza na kusitishwa mzingiro wa pande zote wa eneo hilo.

Kiongozi wa harakati ya muqawama ya Ansarullah, Abdul-Malik al-Houthi, amesema ni "heshima na baraka kubwa kukabiliana na Marekani moja kwa moja."

Mashambulizi hayo yamelazimisha baadhi ya makampuni makubwa zaidi ya meli na mafuta duniani kusimamisha usafiririshaji wa mizigo yao kupitia mojawapo ya njia muhimu zaidi za biashara ya baharini. Sasa baada ya kufungwa Bahari ya Sham, meli zimelazimika kuongeza maelfu ya maili kwenye njia za kimataifa za baharini kwa kuzunguka bara la Afrika badala ya kupitia Mfereji wa Suez.