Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

8 Aprili 2024

20:13:02
1450079

Kwa nini jamii ya kimataifa imeshindwa kuzuia mauaji ya kimbari ya Israel huko Gaza

Kutokuwa na uwezo jamii ya kimataifa wa kusimamisha mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza kumekosolewa vikali kimataifa.

Mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya watu wa Gaza yameingia mwezi wa saba. Hadi sasa, zaidi ya Wapalestina 33,000 wameuawa shahidi na zaidi ya 75,000 wamejeruhiwa katika jinai hiyo.

Ayatullah Ali Sistani, kiongozi mkuu wa kidini nchini Iraq ameeleza masikitiko yake juu ya kushindwa kwa walimwengu kusimamisha jinai na hujuma zinazoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza. Ahmed El-Tayeb, Sheikh wa Al-Azhar pia ameikosoa jamii ya kimataifa kwa kutojali jinai zinazofanywa na Israel dhidi ya watu wa Palestina na kutangaza kwamba: "Tunayoyashuhudia huko Gaza yanathibitisha kwamba, ulimwengu wetu wa sasa umepoteza uongozi wa hekima na busara, na hili linaielekeza dunia kwenye shimo ambalo historia haijawahi kuona mfano wake."

Sheikh wa Al-Azhar ameashiria maazimio yasiyo na maana yoyote yaliyotolewa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kukomesha mashambulizi na uvamizi wa Israel dhidi ya Gaza na kutotekelezwa maamuzi yoyote ya kimataifa kuhusiana na suala hili, akisisitiza kwamba taasisi za kimataifa zimepooza na kudumaa baada ya maamuzi yao kufutwa kwa uingiliaji wa wazi wa upande mmoja dhalimu na wa kimabavu. 

Swali muhimu linalojitokeza ni kwamba, kwa nini jamii ya kimataifa imeshindwa kukomesha mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel huko Palestina?

Inaonekana kwamba jibu muhimu zaidi la swali hili ni matumizi mabaya ya haki ya kura ya veto ya Marekani katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Katika kipindi cha miezi sita iliyopita, Marekani imesimama bega kwa bega na utawala wa Kizayuni na Israel, na mbali na misaada ya kijeshi na kiuchumi, imezuia kupitishwa aina yoyote ya azimio la kulaani jinai zinazofanywa na utawala huo huko Palestina. Utumiaji mbaya wa kura ya veto unaofanywa na Marekani umethibitisha kwa mara nyingine kwamba haki hiyo imekuwa chombo cha kisiasa kinachozuia kupatikana kwa haki na uadilifu katika mfumo wa dunia.

Jambo lingine muhimu ni kwamba, maazimio ya Baraza la Usalama la UN pia yanakosa dhamana ya utekelezaji wake. Kwa mfano tu, hivi karibuni Baraza la Usalama la UN lilipasisha azimio lililosusiwa na Marekani, la ulazima wa kusitisha mapigano mara moja huko Gaza na kutumwa misaada ya kibinadamu katika eneo hilo; lakini baraza la mawaziri la Israel lilitangaza rasmi kwamba litapuuza azimio hilo na halitalitekeleza. Kwa hiyo, inaweza kusemwa kuwa maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hayatakuwa na hakikisho la utekelezaji maadamu mataifa ya Magharibi, hasa Marekani, hayataki. 

Sababu nyingine muhimu inayoifanya jamii ya kimataifa ishindwe kusimamisha mauaji ya kimbari ya Israel huko Gaza ni mwenendo wa nchi za Waislamu. Kwani, licha ya mauaji ya kimbari yanayoendelea huko Gaza, inasikitisha kwamba, nchi za Kiislamu zimeshindwa kuwa na msimamo mmoja wa kukabiliana na utawala wa Kizayuni na kuitetea Palestina. Baadhi ya nchi muhimu za Kiislamu zimekaa kimya na baadhi nyingine hazikutaka hata kumhoji balozi wa utawala wa Kizayuni katika nchi hizo. Katika hali kama hii, utawala wa Kizayuni umefikia hitimisho kwamba, inawezekana kuendeleza mauaji ya kimbari huko Gaza. Hapana shaka yoyote kwamba, iwapo kutakuwa na umoja baina ya nchi za Kiislamu katika kuilinda na kuitetea Palestina, basi utawala wa Kizayuni wa Israel hautaweza kuendeleza mauaji hayo ya kimbari.


342/