Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

8 Aprili 2024

20:14:35
1450082

Kiongozi Muadhamu awataka wanafunzi wawe na mtazamo wa ukosoaji

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameutaja mustakabali bora kuliko leo kuwa ndio lengo kuu la nchi na mfumo wa Kiislamu, na kutoa wito kwa wanafunzi na jumuiya za wanafunzi kuwasilisha masuluhisho mapya ili kufikia lengo na maendeleo haya ya kimsingi bila kudorora nchi kimaada na kimaanawi.

Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyasema hayo Jumapili jioni mjini Tehran katika kikao na wanafunzi wa vyuo vikuu na wawakilishi wa makundi ya kisiasa, kijamii, kiutamaduni na kisayansi katika vyuo vikuu. Amesema mazingira ya wanafunzi huwa ya furaha, yenye uchangamfu, ya kusisimua, yenye shauku na kuwasilisha matakwa na kuongeza kuwa, 'mapendekezo ya wanafunzi yanapaswa kuwa ya kina kwa mtazamo wa kifikra na yenye kuzingatia uhalisia wa mambo ili kusaidia kutatua matatizo."

Ayatullah Khamenei ameutaja mwezi mtukufu wa Ramadhani wa mwaka huu kuwa ni mwezi mzuri katika suala zima la mwonekano wa mandhari kiroho na kimaanawi katika jamii ikiwemo kuenea kwa vikao vya kusoma Qur'ani na hivyo  amewausia wanafunzi kudumisha nuru na utakasifu unaopatikana katika mwezi huu ili kufikia lengo kuu ambalo ni kuepuka dhambi.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema wakati kunakuwepo na kughafilika kuhusu namna baadhi ya matendo huwa dhambi, hiyo huwa sababu ya kuendelea na matendo hayo. Amesema: "Baadhi ya mazungumzo na maandishi katika mitandao ya kijamii hufanyika bila ya utafiti na mazingatio na huo ni mfano wa madhambi ya kughafilika na kila mtu lazima awajibike mbele ya Mwenyezi Mungu."

Ayatullah Khamenei amemtaja mwanafunzi wa chuo kikuu kuwa ni kijana, mwenye nguvu na mwenye ari, mtu wa elimu na fikra na mwenye mustakabali na akasema: "Kwa kuzingatia sifa hizo, wanafunzi wanatarajiwa kuwa wachamgamfu na hasa kuhusu mustakabali."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Malengo ya Jamhuri ya Kiislamu yanaweza kufupishwa chini ya vichwa viwili vya jumla vya "kusimamia nchi kwa msingi wa mafundisho ya Kiislamu" na "kuwa kigezo kwa watu wa dunia kuhusu utawala bora wa nchi."

Amesema katika vikao vya kielimu wanafunzi wa vyuo vikuu wanapaswa kujitahidi kuwasilisha njia mpya za kufikia malengo hayo mawili. Ameongeza kuwa: "Kuendesha nchi kwa njia ya Kiislamu maana yake ni kuwa kwenye njia ya kimaada na kimaanawi bila ya kurudi nyuma." Aidha amesema ustawi wa jumla, usalama wa kimwili na kimaadili, maendeleo ya kisayansi, ustawi wa afya, kuhakikisha jamii inabakia kuwa changa, ubunifu, na haki ni nukta za msingi katika maendeleo ya kimaada. Ayatullah Khamenei pia ameitaja elimu kuwa nguzo kuu ya chuo kikuu na kusisitiza kazi tatu kuu za chuo kikuu, yaani "kumsomesha mwanachuoni", "kuzalisha elimu" na "kutoa mwelekeo wa kuibua mwanachuoni au msomi aliyeboboea na uzalishaji wa elimu." 

 Amesema vyuo vikuu vingi vina tatizo katika nukta ya tatu, yaani kuibua wanachuoni na kuzalisha elimu na kwa sababu hii, hutumiwa na madola ya kiistikbari na Wazayuni. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa sekta zote za chuo kikuu ikiwa ni pamoja na wasimamizi, maprofesa, wanafunzi na vitabu zinapaswa kutumikia nukta hizo tatu. Amesema kuzingatiwa nukta hizo ni sababu muhimu ya Iran kupata heshima ya kimataifa kutokana na maendeleo ya kisayansi na kiteknolojia na kuongeza kuwa: "Kwa kudumisha heshima hii, Iran itaweza kustawi kisayansi na bila shaka, madola ya kiistikbari hayapendi kuona Iran ikiwa na nguvu na heshima."   

342/