Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

8 Aprili 2024

20:15:04
1450083

Iran ni kisiwa cha utulivu katika eneo la Asia Magharibi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian amesema Iran ni kisiwa cha utulivu na usalama katika eneo lenye matatizo la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati).

Amir-Abdollahian aliyasema hayo katika mkutano na waandishi wa habari akiwa na mwenzake wa Oman Sayyid Badr Al-Busaidi mjini Muscat siku ya Jumapili.

Amesema Iran haitamruhusu mtu yeyote kudhoofisha usalama wake wa taifa na kuongeza kuwa Tehran imetuma ujumbe wa wazi kwa Marekani kufuatia mashambulizi ya Israel dhidi ya ubalozi mdogo wa Iran nchini Syria Jumatatu iliyopita na kubaini wazi  kwamba Washington haiwezi kukwepa jukumu lake la shambulio hilo.

Amesema Iran itaendelea kuimarisha uhusiano wake na majirani zake katika nia ya kusaidia kupanua usalama na maendeleo katika eneo hili.

Ameishukuru Oman kwa jukumu ambalo nchi hiyo ya Kiarabu imechukua kusaidia kuondoa msururu wa vikwazo vya upande mmoja vilivyowekewa Iran katika miaka ya hivi karibuni.Amir-Abdollahian amesema Iran na Oman zimeazimia kuboresha uhusiano wao wa kiuchumi na kibiashara kwa kuzingatia ushirikishwaji zaidi wa sekta binafsi za nchi hizo mbili.

Amesema kuanzishwa kwa ukanda wa usafiri wa Kaskazini-Kusini unaounganisha Uzbekistan na Turkmenistan hadi Oman kupitia Iran kutahudumia maslahi ya nchi zote zinazohusika na mradi huo.

Hali kadhalika amesema Iran na Oman zina msimamo wa pamoja kuhusu haja ya kukomesha mgogoro wa kibinadamu huko Gaza ambapo utawala wa Israel umehusika katika miezi sita ya hujuma za kinyama dhidi ya Wapalestina.

Kwa upande wake, Busaidi amesema kuwa Oman inaiona ziara ya Amir-Abdollahian mjini Muscat kama fursa ya kukuza uhusiano wa pande mbili na kikanda.

Amesema Iran na Oman zitajitahidi kufanya kazi pamoja kutafuta suluhu ya mivutano na migogoro ya kieneo, hasa vita vya Israel dhidi ya Gaza ambavyo amesema vimesababisha maumivu na mateso makubwa kwa watu wa eneo hilo.



342/